The House of Favourite Newspapers

Serikali: Si Kila Tatizo la Kupumua ni Corona

0

KATIBU Mkuu8 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe, amewatoa hofu wananchi kwamba matatizo katika mfumo wa kupumua sio kuumwa ugonjwa wa corona (Covid-19).

 

 

Ametoa elimu hiyo jana wakati akiongea na waandishi wa habari, baada ya ziara yake katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando,  na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza  ya Sekou Toure, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya nchini.

 

 

“Watu wasiogope kwenda hospitalini, siyo kila wagonjwa ambao wanahitaji huduma ya mfumo wa hewa wanahitaji kupewa utambuzi (diagnosis) kuwa na ugonjwa wa Corona, kuna wenye kisukari, kuna wenye matatizo ya moyo na wenye presha na wakina mama wajawazito,” amesema.

 

 

Aliendelea kusema kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure ina jumla ya vitanda 315, huku wagonjwa watano ambao wamelazwa wakisumbuliwa na magonjwa ya kisukari na moyo, huku akisisitiza kuwa wagonjwa wote wamegunduliwa kuwa na hali hiyo baada ya kufika hospitali.

 

 

“Sekou-Toure ina vitanda 315, lakini kuna wagonjwa watano ambao wamelazwa wakiwa na magonjwa ya sukari, magonjwa ya moyo, na wote hawa wamegunduliwa na kisukari wakiwa hospitalini jambo ambalo ni hatari katika afya ya binadamu,” amesema.

 

 

Aidha, Prof. Mchembe amewataka wananchi kujenga tabia ya kujitokeza kupima afya zao mapema ili kutambua hali zao na kuweza kupata matibabu bila ya kuchelewa kabla ya kupata matokeo ya hali ya kushindwa kupumua.

 

 

“Ningeshauri jamii kujitoa mapema kupima afya zetu hata kabla ya kuwa na matokeo kama haya, kwa sababu kushindwa kupumua hakuendani na sababu moja tu ya kwamba umepata maambukizi ya mfumo wa hewa, inawezekana isiwe mfumo wa hewa na ikawa moyo ndiyo una tatizo, au sukari imepanda, na vyote vinapelekea tatizo la kupumua,” amesema.

 

 

Pia, amewataka watoa huduma kuwahudumia wananchi wa aina zote, huku akiamini katika hali ya utoaji huduma kwenye hospitali hiyo hakuna mtoa huduma anayehofia mgonjwa mwenye tatizo la mfumo wa kupumua kwamba ana ugonjwa wa corona.

 

 

Leave A Reply