The House of Favourite Newspapers

Shilole Sasa ni Bosi Aliyeajiri Wengi

0

MPENZI msomaji, natumai umzima wa afya na unaendelea kupambania mkate wako wa kila siku. Wiki iliyopita tuliona namna Shishi Baby alivyoteseka na ujauzito hadi kuingia stendi ya mabasi pale Igunga na kuanza biashara yake ya mikate na maji hadi akafanikiwa kufikia uwezo wa kupanga chumba cha shilingi 3,000 na kujifungua salama.

 

SASA TWENDE PAMOJA…

WAKATI maisha yakiwa ya kuungaunga, Shilole alibahatika kupata mchumba akiwa bado na umri wa miaka 17, walitokea kupendana mno kisha mwanaume huyo kufuata taratibu zote za kuwaona wazazi na ndugu wa shilole na kutoa mahali na baadaye ndoa ikapita salama.

 

Kwa kuwa mumewe huyo alikuwa ni dereva wa magari makubwa ya mizigo yaendayo mikoani, basi alimuomba Shishi waende kuishi wote Dar. Shilole akakubali. Hapo ndipo safari ya Shishi kutinga Dar ilipoanzia.

 

Binti ambaye hakuwahi kuwaza kufika jiji kubwa kama Dar, wala hakuwa na ndugu Dar, aliingia mjini! Huku wakifikia katika nyumba ya kulala wageni iliyopo maeneo ya Keko, waliishi hapo kwa kipindi cha miezi kadhaa hadi mumewe alipopata pesa na kutafuta nyumba ya kupanga kisha kuhamia huko.

 

Ni kama malaika alitumwa kule Igunga kumchukua Shishi na kumleta Dar ili authibitishie ulimwengu kuwa; hata kama unatokea familia duni kiasi gani, hata kama hakuna mtu aliyefanikiwa katika ukoo wenu. Hata kama baba na mama hawakuwahi kuuvuka mstari wa umaskini, lakini wewe unaweza kuwa tajiri na mwenye maisha mazuri. Kama una pumzi, Hakuna linaloshindikana chini ya jua.

 

Baada ya miaka kadhaa ya furaha na amani kwenye ndoa yake, Shilole alianza kupata vipigo mara tu baada ya kujifungua mtoto mwingine kutoka kwa mumewe.

 

Ilifikia hatua Shishi Baby alikuwa analala kituo cha Polisi na watoto wake ili tu kukwepa vipigo vya mumewe huyo.

Cha kushangaza, Shishi hakuwaza kurudi nyuma tena, hakutaka kurudi Igunga kupamabana na mikate pale stendi huku jua likimpiga.

Alitafuta ada kisha kujiunga na chuo cha utalii ambapo alisoma kwa juhudi zote na Mungu alisaidia, maana alipomaliza tu chuo aliajiriwa katika hoteli moja jijini Dar.

Mumewe hakupendwezwa na hatua hiyo ya Shishi hivyo alichukua uamuzi wa kumpa talaka na kumtupia vitu vyake vyote nje.

 

Asichokuwa anakijua, kumbe ni kama alikuwa anampiga chura teke au anamtoa nyangumi kwenye bwawa na kumruhusu aende kukua baharini.

Naam, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwanamama Shishi, maana akiwa anafanya kazi hotelini, alikutana na nguli wa sinema za Kibongo, Ray Kigosi na hapo ndipo milango ikafunga.

 

Baada ya Shishi kumueleza Ray kuwa anapenda kuigiza, basi alipewa nafasi na kwa mara ya kwanza alishiriki katika Filamu ya Fair Decision ya mwaka 2010.

 

Baadaye, Shishi alikutana na msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Q Chief ambaye alimpeleka hadi kwa Producer C9; mtayarishaji wa muziki na akafanikiwa kutoa wimbo wake wa kwanza unaojulikana kama Lawama.

Katika harakati zake, Shishi alikutana na Ruge (R.I.P) ambaye alionesha kumpa sapoti kubwa katika kuzifikia ndoto zake.

 

Niliwahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja, kwa nini watu wengine wanafanikiwa mapema na wengine hatufanikiwi kabisa? Mimi nilimjibu; Ongea na watu vizuri, watu ndiyo ngazi na nguzo muhimu katika mafanikio ya wengi.

Unaweza kuutathimini msemo huo kwa namna Shishi alivyoshikwa mkono na watu; watu ambao hata hawakuwa wakitokea sehemu moja wala kujuana kabla.

 

Binti aliyebakwa na kukatishwa masomo akiwa anatokea katika familia duni zaidi, leo ni maarufu ndani na nje ya Tanzania. Nani asiyemjua Shishi? Nani?

 

Sasa mwanamama huyo anamiliki mgahawa wake wa chakula wa Shishi Food uliopo Ada Estate, Kinondoni jijini Dar na Dodoma Mjini ambao unawalisha mastaa kibao Bongo na viongozi wakubwa wa Serikali.

Sasa Shishi anamiliki nyumba kule Kivule jijini Dar na magari yake binafsi!

 

Wakati mwingine sababu ya mtu kutofanikiwa ni visingizio vingi alivyonavyo ambavyo vinamuaminisha kuwa vina mashiko. Fikiria mtu kama Shishi angesema; “Nimebakwa nikiwa na umri mdogo, nimepata mimba na kukatishwa masomo nikiwa kidato cha pili, nilikosa baba mzazi wa kunilea, nilipigwa na kuachwa na mume wangu, sikuwa na ndugu mwenye pesa na visingizio vingine kama hivyo.

 

Visingizio hivi vyote vingemuaminisha kuwa ni sababu zenye mashiko za kushindwa na kutofanikiwa kwake. Lakini Shishi hakutaka kufanya visingizio hivyo viwe sababu ya yeye kutofanikiwa. Leo Shishi ni bosi mkubwa aliyeajiri wengi.

 

Toleo lijalo, tutakuwa na Harmonize; namna alivyotoboa tundu kutoka Kijijini Tandahimba kule Mtwara hadi kukamata mashabiki Marekani, usikose!

Makala: BAKARI MAHUNDU

 

Leave A Reply