Shoga; ukisemwa na mumeo usinune, itakula kwako!

Shoga yangu, leo ni Jumanne nyingine ambapo tunakutana katika safu yetu hii ambayo tunaitumia kukosoana na kuelimishana kuhusu masuala ya ndoa nk.

Baada ya wiki iliyopita kuzungumza nawe kuhusu mada iliyosema ‘mumeo umepewa na Mungu jiachie utakavyo,’ leo nataka kukutahadharisha kwamba ukisemwa na mumeo usinune, itakula kwako.

Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya wenzetu wana tabia ya kupenda kuwanunia waume zao inapotokea wamesemwa baada ya kuzembea eneo f’lani.

Tena wanafanya hivyo, hata kama waume zao wametumia lugha ya kawaida tena wakiwa peke yao chumbani, shoga kufanya hivyo ni kukosea.

Shoga yangu, wanandoa kukosoana kwa lengo la kuwekana sawa ni jambo zuri sasa inapotokea mumeo kakusema kwa kushindwa kupika kwa wakati, kufua nguo, kuchelewa kurudi nyumbani nk usimnunie.

Wapo ambao huwanunia waume zao zaidi ya siku tatu hata wiki na kusitisha huduma zingine kwa mumewe kama kumuwekea maji ya kuoga, kumwandalia nguo za kuvaa, kumpokea chochote anachorejea nacho nyumbani kutoka kazini.

Ukiacha hayo, mama aliyeamua kununa hayuko tayari kushirikiana na mumewe katika yale mambo yetu ya chumbani zaidi na kuishia kulala mzungu wa nne kama mtu na dada yake.

Najiuliza nashindwa kupata jibu sababu hasa inayomfanya mwanamke aliye kwenye ndoa kumnunia mumeo kisa kamsema kwa lengo la kumuweka sawa au baba kuchelewa kurudi nyumbani nk.

Tabia hiyo shoga yangu haijakaa sawa kwani inaweza kusababisha mumeo kuchepuka ili kuifurahisha nafsi yake kisa wewe kununa. Bye!


Loading...

Toa comment