The House of Favourite Newspapers

SIKU WALIYOZALIWA WANANGU ILIKUWA MBAYA

0
SIKU WALIYOZALIWA WANANGU ILIKUWA MBAYA
Siku mbaya

NAIKUMBUKA siku hiyo, hata naogopa kuitaja. Ni siku waliyozaliwa wanangu mapacha – Kisiki na Mpingo.

 

Niliondoka asubuhi ya siku hiyo kwenda ofisini kutimiza majukumu yangu ya kila siku. Nilimuaga mke wangu aliyekuwa mjamzito na dalili zilionesha wazi kuwa angejifungua siku yoyote.

 

Nilipofika ofisini sikuamini nilichokiona, moshi mkubwa ulifuka katika jengo la ofisi niliyofanya kazi. Moto ule uliteketeza ajira yangu ya kudumu niliyoitegemea. wakati nikiendelea kuzubaa, simu yangu ikaita, nikapokea haraka, “hallo sema dada.”

 

Nilipewa taarifa kuwa mke wangu aliwahishwa hospitali kwa sababu hali yake ilibadilika ghafla. Bila shaka ule wakati wa kujifungua ulifika. Pia niliombwa nitume fedha kwani lolote laweza kutokea, na kwa kuwa hakufahamu kama ofisi yangu iliteketea, alinikumbusha  baada ya kazi nifike hospitali!

 

Niliamua kutuma fedha. Sikuwa nazo mfukoni, nikachomoa kadi ya benki na kusogea katika ‘ATM’. Sikuamini nilichokiona, salio lilikuwa sifuri. Nikakumbuka kuwa jana nilifanya manunuzi ya mtandaoni na bila shaka mtandao ule ulikuwa ‘feki’ hivyo nilitapeliwa. Masikini mimi, ofisi iliungua na fedha ziliibwa!

 

Nilitamani kulia lakini sikuwa na nguvu. Akili ikanituma niende kwa mchepuko wangu laazizi wa mafichoni nikalale kupoza kichwa kilichoanza kuchemka kama pasi. Mguu na njia taratibu kwa unyonge nilifika.

 

Nilikuwa na funguo. Nilifungua mlango taratibu mpaka ndani, nilipoingia nikakuta simanzi nyingine. Mchepuko wangu alikuwa kalala katika sofa, juu yake kalaliwa na jamaa mmoja mwenye ndevu nyingi. Walishituka wakanitazama. MCHEPUKO ULIKUWA UKICHEPUKA.

 

Nilimtambua mwanamme yule. Alikuwa Bwana Teke. Bwana huyu alikuwa ananidai fedha nyingi na nilikuwa nikimzungusha. Deni hili lilipunguza nguvu ya kulalamika. Hata hivyo nilijikaza kiume nikafyatua maneno, “We mwanamke achana na mimi, sitaki tena michepuko. Bwana Teke tumemalizana! Fedha zako sikulipi.”

 

Niliondoka taratibu nikaikamata njia nyembamba iliyoelekea nyumbani kwangu. Kichwa kilikuwa kizito. Nilihitaji kupata sehemu ya kujituliza.

 

Mshituko mwingine ulinipata nilipofika nyumbani. Sikuikuta nyumba, nilikuta kifusi… walikwishabomoa nyumba yangu, nilijenga katika hifadhi ya barabara, na waliweka alama  ya X kwa muda mrefu. Sasa walitimiza.

 

Nikiwa katika dimbwi la simanzi nzito, nilipokea simu kutoka kwa dada, “Mkeo kajifungua watoto mapacha! Tuma fedha.”

 

 

 

Leave A Reply