The House of Favourite Newspapers

Simba: Mbeya City mmekuja wakati mbaya

Said Ally na Omary Mdose | CHAMPIONI| DAR ES SALAAM

SIMBA leo Jumamosi inacheza na Mbeya City mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, klabu hiyo imesema wapinzani wao wamekuja wakati mbaya kwao. Kocha wa Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, amesema Mbeya City imekuja kipindi ambacho timu yake inataka ushindi kwa lazima ili wawe katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Omog alisema pia Mbeya City inakutana na beki Juuko Murshid ambaye hakuwepo kikosini tangu kuanza kwa mwaka huu. Juuko, raia wa Uganda, Januari, mwaka huu, alikuwa Gabon akiiwakilisha nchi yake katika Kombe la Mataifa ya Afrika. Simba ina pointi 54 kileleni mwa ligi hiyo ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 52, wakati Mbeya City ikiwa nafasi ya nane na pointi 29 huku Mtibwa Sugar ikiwa na pointi 33 katika nafasi ya tano.

“Wapinzani wetu wamekuja wakati mbaya sana, kwani sisi tunasaka pointi tatu kwa juhudi zote ili wasipotee katika mbio za ubingwa, pili ni kurejea kwa beki wetu Juuko. “Safu yetu ya ulinzi imeimarika kuweza kupambana na timu yoyote.” Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, raia wa Malawi, alisema: “Tumejipanga kushinda mchezo huu, kikosini tuna nyota wengi wenye uzoefu, tutawatumia kuifunga Simba.”

YANGA YAIPANIA MTIBWA

Kesho Jumapili Yanga itacheza na Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ambapo kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, naye amesema hahofii lolote katika mechi hiyo. Lwandamina alisema: “Tunataka kushinda kila mchezo, kuelekea mwisho wa msimu hatutakuwa tayari kupoteza hata moja pointi, tunajua tutakuwa ugenini dhidi ya Mtibwa, lakini hilo hatulihofii.

“Tunachotakiwa kukifanya sasa ni kuwakimbiza waliokuwa juu yetu mpaka mwisho wa msimu ili tuone inakuwaje kwa sababu tunahitaji ubingwa na ubingwa hauji hivihivi bila ya kushinda na kupata pointi.” Kwa upande wake Kocha wa Mtibwa, Shaban Katwila, alisema:

“Tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mchezo huo, tutahakikisha tunaifunga Yanga ili kuleta matumaini mapya kikosini mwetu.

“Tunajua Yanga ina wachezaji wengi hatari kama Msuva (Simon), lakini hatutamuogopa yeyote, tumeweka ulinzi wa hali ya juu kuhakikisha wachezaji wa Yanga hawatusumbui.”

Comments are closed.