The House of Favourite Newspapers

Simba vs Yanga ‘Zinawatesa’ Mastaa Mitandaoni

0

SOKA ni moja kati ya michezo inayoongoza kwa kupendwa. Kuwa shabiki wa mpira ni kama vile kile kilevi, huachi kutaka kufuatilia. Kibongobongo wapo mastaa ambao ni mashabiki wa soka lakini mara nyingi hawapendi kuonesha hisia zao, lakini wapo wasanii ambao wao ni walevi kweli kweli wa soka.

 

Kwa wapenzi hao wa soka, wamejikuta wakitukanwa kweli na mashabiki pinzani pindi wanapoonesha hisia zao kwenye mitandao ya kijamii.Mastaa hawa wamegawanyika kwenye sehemu mbili; Yanga na Simba ambazo kesho zinakutana kwenye Uwanja wa Taifa katika Kombe la Shirikisho (FA).

Tuwaangalie mastaa hao ambao kujilipua kwao mitandaoni, kunawapa mateso makubwa pindi mambo yanapokuwa mabaya kwa klabu zao:

 

KIBA-YANGA

Mbali na kwamba ni msanii na mtunzi mzuri wa mashairi, lakini pia ana kipaji kingine cha kucheza soka, miaka kadhaa iliyopita Coastal Union ya Tanga walimsajili kucheza mpira wa miguu kwa msimu wa 2018/2019 wa Vodacom Premier League.

 

Aidha, msanii huyo amekuwa ni mpenzi wa mpira wa miguu na mara kadhaa amekuwa akiipenda na kuishangilia sana klabu ya soka ya Yanga na inaelezwa kuwa, alianza soka zamani na kufanikiwa kuchezea vilabu kadhaa kabla ya kuingia kwenye muziki.

 

MONDI-SIMBA

Ukiambiwa utaje mastaa watatu Bongo wanaofanya vizuri kati iwanda cha muziki, basi naamini hautaacha kutaja jina la mtoto wa Tandale, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye kadiri siku zinavyozidi kwenda, ndivyo ambavyo anazidi kuleta mapinduzi kwenye gemu.

 

Licha ya kwamba mara kadhaa amekuwa akisema hana timu na wala yeye sio shabiki wa mpira, lakini Septemba 2019, msanii huyo alibadili mawazo yake na kujikuta akiwa mpenzi wa mpira ambapo alisema yupo katika mazungumzo na mchezaji maarufu wa mpira kutoka Cameroon Samuel Eto’o kutaka kujenga shule ya mpira nchini humo.

 

Aliendelea kusema kwamba, hapo awali alifikiri kuwa masuala ya michezo ni kitu kisichokuwa na faida, lakini kumbe ni jambo lenye faida sana, hivyo huko mbeleni atakuwa mmiliki wa timu yake yeye mwenyewe, ambayo tayari inafanya biashara kwenye Premier.

 

Aidha, msanii huyo amewahi kukaririwa akisema kuwa, hawezi kujiita Simba halafu akashabikia Chui, hivyo lazima watu hasa mashabiki zake watambue kwamba yeye anapenda timu gani.“Siku zote unajua siwaambiagi watu mimi ni timu gani, siwezi kujiita Simba nikashabikia Chui, mimi ni Simba na timu yangu ni Simba,” anasema Mondi.

 

WEMA-YANGA

Ni mwanamke mrembo haswa, lakini mbali na sanaa ya uigizaji anayofanya, pia mwanadada huyu amewahi kusema kuwa tangu akiwa mdogo, alikuwa na mapenzi makubwa na mpira wa miguu.

 

Mara kadhaa amekuwa akijitapa kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa timu ya Yanga na mchezaji anayempenda na kumkubali katika timu hiyo ni Haruna Niyonzima kwa sababu ya uwezo wake anao uonyesha uwanjani.

 

MOBETO-SIMBA

Ni mwanamitindo na msanii wa Bongo Fleva, huyu ni shabiki lialia wa Simba. Anatupia picha kibao akiwa uwanjani pale Simba inapoche.

 

RAY-YANGA

Ni staa wa Bongo Muvi, lakini naye ni shabiki mkubwa wa timu ya Yanga, humuambii kitu kuhusu Yanga.Amekuwa akiisapoti kila wakati na amekuwa akipambana kuonesha ubora wa timu hiyo licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.

 

JB-SIMBA

Mbali na kuwa yupo vizuri kwenye filamu zake, msanii huyu amekuwa akijitoa vilivyo kuisapoti Simba. Si tu kwa kuangalia kwenye runinga, bali anaingia hadi uwanjani na kutupia uzi wake mwekundu.Mapenzi yake na klabu ya Simba ni makubwa, hali iliyopelekea kuwa na upinzani mkubwa na Ray pale linapokuja suala la Simba na Yanga kwa kuwa wamekua timu mbili tofauti.

 

MWANAFA-SIMBA

Huyu ni gwiji wa muziki wa Hip Hop Bongo, lakini naye amekuwa na mahaba na timu ya Simba kiasi kwamba huwezi ukamwambia kitu kuhusu timu hiyo akakuelewa. Ni rafiki mkubwa wa bosi wa Simba, Mohamed Dewji na wamekuwa mara kadhaa wakionekana gym pamoja na uwanjani.

 

MONALISA-SIMBA

Ni staa wa Bongo Muvi, anajua kuipenda Simba. Ana mabaha kwelikweli na Simba, ikitokea imepoteza mchezo, anaumia kwelikweli na hasa mastaa  wenzake wanavyo msha mbulia mitandaoni.

 

DAVINA-YANGA

Huyu naye ni msanii wa filamu nchini lakini humwambii kitu kuhusu mpira wa miguu, anaipenda Yanga kufa. Mara kadhaa amekuwa akionekana kuishabikia timu hiyo, na hata uwanjani kila mara inapocheza.Ikitokea Yanga imepoteza, huwa anaumia na wenzake wa Simba wamekuwa wakimtania sana maana huwa anashiriki sana kwenye kampeni mbalimbali za kuhamasisha michezo ya Yanga.

 

STEVE NYERERE-YANGA

Huyu ni Yanga damu. Mara kadhaa wamekuwa wakipeana maneno ya ‘kuudhi’ na Msemaji wa Simba, Hajji Manara. Anaipenda Yanga, amekuwa akiipigania kwelikweli hata pale inapoboronga, bado anaendelea kupambana na mashabiki wa Simba mitandaon.

Leave A Reply