The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kassim Kayira : Akaa nyumbani siku tatu tu baada ya kuacha kazi! 8

0

kassim kayiraMBIO za kusaka mafanikio maishani ni ndefu mno. Inakuhitaji kuwa mpambanaji haswa, tena usiyekata tamaa mapema.

Kassim Kayira ni mmoja wa watu waliobadili maisha yao kwa kupambana. Safari yake ya kuyafikia maisha anayoishi kwa sasa, ilikuwa ngumu lakini kwa sababu ya uvumilivu, leo anaishi maisha mazuri. Anapata kila kitu, anafurahia utajiri na umaarufu mkubwa.

Wiki iliyopita, aliishia kusimulia jinsi alivyoamua kuacha kazi katika shirika la utangazaji nchini Rwanda, baada ya kuhamishwa kikazi kutoka jijini Kigali hadi kijijini, baada ya kuvumbua na kuripoti ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa na wabunge, mawaziri pamoja na watumishi wengine wa serikali.
Je, nini kilifuata?
ENDELEA…

“Nataka niweke wazi jambo moja muhimu sana hapa, kuhusu maisha,” anasema Kayira.
“Ndiyo kaka,” najibu na wakati huo nasitisha kuandika, badala yake naacha kifaa cha kurekodia sauti kifanye kazi yake.

“Watu wengi huwa na hofu kubwa sana kuacha kazi kwa kuhofia ugumu wa maisha, hata kama kazi zao ni ngumu na zinawadhalilisha utu wao, lakini bado wanakuwa waoga wa kuachana na kazi hiyo kwa sababu anahofia ataishi vipi baada ya hapo.

“Anakuwa amesahau kabisa kwamba yupo Mungu apangaye riziki, hiyo siyo sawa kabisa katika maisha. Mimi huwa siwezi kuona nadhalilishwa kisa eti kazi ya mtu, naondoka na kazi yako nakuachia, Mungu aliyenileta duniani ndiye atajua nitaishi vipi, kama nitakufa kwa kukosa kazi, sawa. Kote nilikopita kufanya kazi, wanajua kanuni na sheria hii ya maisha yangu.

“Si kwamba najigamba eti au vile naringa, hapana, ila nina msimamo juu ya maisha yangu, pesa zinabaki kuwa zako na maisha yangu yanabaki kuwa yangu. Sipendi kunyanyasika, huko mbele nitakueleza kwa kina mambo mengi sana niliyopitia nikiwa BBC,” anasema mfululizo Kayira lakini kwa lafudhi ya Kiswahili cha Kiganda.

“Basi bwana, kwa hiyo baada ya kuhamishiwa kazi huko kijijini, niliona kabisa hawakuwa na nia njema, hakukuwa na kazi, wameamua kunifukuza kwa ujanja kabisa. Wanakwepa kunilipa fidia kwa kunifukuza kazi, ndiyo maana waliamua kunipeleka kijijini. Nikachukua uamuzi wa kuacha kazi,” anasema Kayira, lakini mazungumzo yetu yakawa yanakatishwakatishwa mara kwa mara na miito ya simu.

“Kumbuka wakati naacha kazi, mke wangu hakuwa na kazi zaidi ya kunitegemea mimi, kwa hiyo akawa na wasiwasi, ingawa kulikuwa na kiasi fulani cha fedha nilichokuwa nimeweka kwa ajili ya akiba,” anasema Kayira.

“Tena nikwambie kitu mdogo wangu, katika maisha yako ya kazi za watu, hakikisha kabisa unaweka akiba ya fedha, hata kama unalipwa mshahara mdogo kiasi gani, weka akiba, huwa haiozi, mimi ilinisaidia baada ya kuacha kazi, hata hicho kiburi cha kuacha kazi, kilitokana na kuwa nimeshajiwekea akiba ya kuendesha familia kwa siku kadhaa wakati nikijipanga upya.

“Siyo leo unaachishwa kazi mahali fulani, kesho yake tena asubuhi tu umeshapiga hodi kwenye ofisi nyingine, hata kama watakuajiri, si kwa kipato kinachoendana na uhalisia hata kama una kipaji na uwezo mkubwa sana, kwa kuwa tu unakuwa umewafuata mwenyewe na ndani huna akiba, familia inakutegemea. Lakini kama una akiba, ofisi zingine wakutafute wewe kutokana na uwezo wako, hapo utaweza kuwatamkia kiasi chochote cha mshahara,” anasema Kayira.

“Kwa hiyo nilikaa nyumbani kwa muda wa siku tatu, lakini nikawa namuomba Mungu afanye jambo maishani mwangu,” anasema Kayira.
“I prayed to God, that was the time I needed him the most”
(Nilimwambia Mungu, kuwa kipindi hicho ndicho nilimhitaji kupita wakati wote),” anasema Kayira kwa Kiingereza.

“Ok, what happened then?”
(Sawa, nini kilifuata),” namuitikia huku nikimuuliza pia.
“Huwezi amini, nilikaa siku tatu tu nyumbani, ndipo Shirika la Inter News, waliokuwa wakishughulika na mambo ya Haki za Binadamu, waliponifuata na kunitaka niwe

awatangazia kipindi chao cha Haki za Binadamu, tukaelewana ambapo walinilipa mara tatu ya mshahara niliokuwa nalipwa na TV Rwanda, maisha yakabadilika ghafla, unaona, That was God On Duty (Mungu alikuwa kazini),” anasema Kayira.
“Mmh, ikawaje?” namuuliza kwa shauku kubwa.
Je, nini kilifuata? Simulizi ndiyo inafika patamu sasa, alifikaje BBC? Usikose kufuatilia tena wiki ijayo.

Leave A Reply