The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kusisimua ya Maisha ya Mkapa

0

MWEZI Novemba mwaka 2019,  Benjamin Mkapa alizindua kitabu juu ya maisha yake, na katika aya ya mwisho ya dibaji aliandika kuwa anatumai kuwa kitabu hicho kitatoa mchango katika historia ya Tanzania na kuwatia moyo na kuwapa maarifa viongozi wa kesho wa Bara la Afrika.

 

Miezi minane toka atoe kitabu hicho, Mkapa ameaga dunia jijini Dar es Salaam na kuacha kitabu hicho kama kumbukumbu yake itakayoishi milele.

 

Historia ya maisha yake, toka alipozaliwa mwaka 1938 na kukua katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Lupaso, mkoa wa Mtwara mpaka kuwa rais ni simulizi ya kutia moyo.

 

Mkapa naeleza namna ambavyo ilimlazimu kutembea kwa umbali mrefu, miguu peku chini, kutafuta elimu katika shule za Wamishenari.

 

Baada ya kumaliza darasa la 10, sawa na kidato cha pili kwa mfumo wa sasa, Mkapa alitaka kuwa askari. Alipoulizwa na mwalimu wake Mzungu kuhusu kuendelea na elimu mpaka darasa la 12 na kisha Chuo Kikuu, Mkapa anakiri kwenye kitabu chake kuwa hakujua kama kulikuwa na muendelezo huo wa masomo.

 

Baada ya kufaulu vizuri darasa la 12, Mkapa alienda Chuo Kikuu cha Uganda ambapo mwaka 1962 alihitimu Shahada ya Kingereza. Baada ya hapo alienda Marekani na kusomea diplomasia.

 

Alifanya kazi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania akianza ajira kama afisa wa wizara ya mambo ya nje na baadaye kuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya chama na serikali pamoja na kuwa mwandishi wa rais Nyerere.

 

Mkapa pia alihudumu katika nafasi ya Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Canada na Marekani. Pia alikuwa waziri wa Mambo ya Nje katika vipindi viwili tofauti katika utawala wa Nyerere na baadaye rais wa pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.

 

Mkapa aliingia madarakani mwaka 1995 baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, baada ya kuhudumu serikalini kwa miongo mitatu.

 

‘Sikutegemea Ungegombea Urais’

Mwaka 1995 Mkapa alijitosa kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pasi kupigiwa upatu na watu wengi.

Katika kitabu chake, Mkapa anaeleza kuwa alimfuata aliyekuwa rais mstaafu wa Tanzania na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kumfahamisha juu ya azma yake ya kugombea urais na sababu zake pia.

 

Mkapa anaandika kuwa baada ya kumsikiliza kwa makini Mwalimu alimjibu kuwa: “…Nitakuwa muwazi kwako. Sikutegemea kuwa ungetaka kuwania urais, wazo kama hilo halikuniingia kabisa.”

 

Lakini si hivyo tu, Nyerere alimweleza Mkapa kuwa kuna mtu mwengine ambaye ailikuwa akimfikiria kuwa angekuwa rais bora, lakini alikuwa akisita kuingia kwenye mchuano huo.

 

“Ben, kitu pekee ninachokuahidi ni kuwa sitakuzibia njia, sitakupinga,” alisema Nyerere/

 

Mkapa alishinda uchaguzi ndani ya chama akipata ushindani mkali kutoka kwa Jakaya Kikwete (ambaye alikuja kumrithi madaraka ya urais mwaka 2005).

 

Alishinda uchaguzi mkuu kwa asilimia 61.8 ya kura, huku kinara wa upinzani katika uchaguzi huo akiwa Augustino Mrema akipata  asilimia 27.7 ya kura.

 

Maboresho ya Kkuchumi

Baada ya kushika hatamu akatekeleza mageuzi ya sera za kiuchumi kwa kubana matumizi, kunyanyua sekta binafsi, kuvutia wawekezaji wa nje na ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

 

Matokeo yake yakawa ni kuungwa mkono na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), na kujenga msingi madhubuti wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa miaka iliyofuata hata baada ya kutoka madarakani.

 

Sera yake ya ubinafsishaji hata hivyo imekosolewa kwa kiasi kikubwa na hata yeye mwenyewe alikiri katika uhai wake kuwa japo nia ilikuwa njema na mafanikio kupatikana lakini sera hiyo ilikuwa na mapungufu pia.

 

Mauaji ya Waandamanaji Pemba

Mkapa ameeleza tukio Januari mwaka 2001 la kuuawa waandamanaji 22 na polisi kisiwani Pemba waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2000 lilmtikisa vilivyo. Alikiri kwenye kitabu chake hicho kuwa tukio hilo litaendelea kuwa doa jeusi kwa utawala wake.

 

Waandamanaji hao walikuwa ni wafuasi wa chama cha upinzani cha CUF ambao walidai mgombea wao Seif Sharrif Hamad alipokwa ushindi. Wakati tukio hilo linatokea Mkapa alikuwa ughaibuni akishiriki mkutano wa kiuchumi.

 

“Yalikuwa ni mauaji mabaya, lakini hakuna hata mtu mmoja ambaye aliangalia ni kwa namna gani polisi walikuwa kwenye shinikizo. Waandamanaji walimuua askari mmoja na kuchoma moto kituo cha polisi,” ameeleza Mkapa.

Mkapa ameandika kuwa anajutia kutokea kwa mauaji hayo japo alidai kuwa suala hilo lilichukuliwa vibaya na nchi pamoja na vyombo vya habari vya Magharibi.

 

Utumishi Baada ya Kustaafu

Hata baada ya kuondoka madarakani mwaka 2005,  Mkapa aliendelea na utumishi kwa nchi yake na jamii ya kimataifa.

 

Uchaguzi wa urais nchini Kenya wa mwaka 2007 ulifuatiwa na ghasia kubwa ambazo zilitishia ustawi wa taifa hilo. Mkapa alikuwa ni mmoja wa viongozi kutoka barani Afrika ambao waliwahi na kuchukua jitihada za kuwaweka pamoja mahasimu wa kisiasa, Raila Odinga na Mwai Kibaki,  katika meza ya mazungumzo.

 

Japo kazi hiyo ya usuluhishi ilikuwa ngumu,  mwishowe ikazaa makubaliano na kuundwa kwa serikali ya mseto na hatimaye kurejesha utulivu nchini humo. Mkapa pia amehudumu kama msuluhishi katika mgogoro wa kisiasa Burundi  na harakati za uhuru za Sudan Kusini.

SAFARI YA MZEE MKAPA, KUZALIWA HADI KIFO NI HISTORIA YA TAMU NA CHUNGU

Leave A Reply