Siri ya Jokate, Makonda kwa Kung’ara Hii Hapa

 

TANGU Rais Dk John Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015 amekuwa akiteua vijana kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini na kuwahimiza kuendana na ari pamoja na kasi aliyonayo katika utendaji wake jambo ambalo sasa limeanza kung’arisha nyota za vijana hao.

 

Licha ya kutokea dosari mbalimbali katika utendaji wa vijana hao, wachambuzi wengi wamechukulia kasoro hizo kama mojawapo ya darasa kwa vijana hao walioteuliwa katika nyadhifa za wakuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala.

 

Tayari Rais Magufuli aliomba vijana anaowateua wavumiliwe kwa baadhi ya matendo yao kwani damu zao zinachemka.

 

“Nimeteua sana vijana, inawezekana kuna makosa watakayokuwa wanayafanya ni kwa sababu ya kuchemka damu, naomba muwavumilie” alisema Magufuli.

Aidha, alisema vijana aliowateua ni hodari na wachapakazi wanaomuwakilisha vema pia, hivyo wasikatishwe tamaa bali wasonge mbele.

 

Hoja hizo za Rais Magufuli sasa zimeanza kudhihirika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kwa kuchapa kazi kwa kasi na ari ambayo sasa matunda yake yanaonekana katika wilaya hiyo.

 

“Leo Jokate ni mpya zaidi, haya yote ni matunda ya kufanya wema uliopitiliza, ukifanya wema Mungu anakupa nuru usoni mwako hata ukipaka mafuta ya nazi watu wanaona unang’aa tu,” alisema Jafo na kumuomba Rais Magufuli amuone zaidi Jokate.

 

Aidha, kwa upande wake Jokate alipokea pongezi za Jafo na kubainisha kuwa ni nadra sana kwa viongozi wa kisiasa hasa vijana kutamka wazi na kukubali kazi ya kiongozi mwenzao hadharani.

Umahiri wa utendaji huo wa Jokate ambaye aliteuliwa miaka miwili iliyopita, unashabihiana na wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokana na ubunifu pamoja na weledi katika utendaji wao.

 

Ubunifu huo unadhihirika wazi kutokana na miradi mbalimbali waliyoianzisha katika sehemu zao za kazi ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji yakinifu wa miradi husika.

 

Kwa mfano hivi karibuni Jokate alianzisha kampeni ya kutokomeza zero katika wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kutokomeza utoro mashuleni. Pia alianzisha kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia katika eneo hilo jambo ambalo limekuwa na mapokeo chanya kwa kila mara kuripotiwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika vituo vya polisi wilayani humo.

 

Vivyo hivyo kwa Makonda ambaye mbali na kufanya ziara, kusikiliza kero za wananchi, pia amebuni miradi mbalimbali ikiwa ujenzi wa majengo ya akina mama kujifungulia, kuanzisha kampeni za kusikiliza kero za akina mama waliotelekezewa watoto, kuwasaidia walemavu kupata miguu bandia, kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na mambo mengine.

STORI | GABRIEL MUSHI, RISASI


Loading...

Toa comment