The House of Favourite Newspapers

Sirro: Tumebaini Mmiliki na Dereva wa Gari Iliyomteka Mo Dewji – Video

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro,  amesema jeshi lake limelitambua  gari  lililotumiwa katika kumteka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (Mo) ambalo lilitokea nchi jirani na kuingia nchini Septemba 1, 2018 na kwamba tayari wamembaini mmiliki wa gari hilo na dereva aliyekuwa akiliendesha.

IGP Sirro amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari  makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

 

“Ni kweli kulikuwa na CCTV Camera, na baada ya tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji kufanyika, tulikamata risasi mbili za bastola ambazo tumezifanyia uchunguzi kwenye maabara yetu ya forensic na kubaini zina ukubwa wa milimita 9. 

 

“CCTV camera zimetusaidia, tumeweza kulitambua gari; hatulikutambua siku hiyo kwa sababu ilikuwa asubuhi. Tumefuatilia na kubaini lilitoka Colosseum likaingia Barabara ya Ally Hassan Mwinyi hadi round about ya Kawe. Watu wetu bado wanafuatilia kuona kama waliingia maeneo ya Silver Sand au maeneo ya Kawe. Tunaamini pale ndipo lilipopotelea gari hilo, hivyo  tutakwenda apartment kwa apartment kwa ajili ya uchunguzi.

 

“Tulipata taarifa kwamba gari hili lilitokea nchi jirani, tumechunguza na kubaini gari la aina hiyo lilipita kwenye mpaka Sept. 1, 2018. Tumewasiliana na wenzetu wa Interpol, tumembaini mwenye gari, nchi anayotoka na dereva aliyekuwa akiendesha.

 

“Wananchi wamekuwa wakitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa Mo Dewji anapatikana, na nitoe rai kwa wenye uwezo wa kuwa na silaha na wenye uwezo wa kifedha wawe na silaha zao, unaweza ukafanyiwa uhalifu ukajihami, au wawe na wasaidizi wao,” alisema Sirro.

 

Aliendelea kusema kwamba ilikuwa ni kawaida kwa Mo Dewji kutembea na silaha lakini siku hiyo hakuwa nayo na kwamba hakuwa hata na dereva wake na ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa waliomteka kufanya hivyo.

Pia Sirro aliwalaumu wananchi wanaotoa taarifa za uwongo kwa jeshi lake kuhusiana na utekaji huo kwa ajili ya mategemeo ya kubahatisha kupata fedha iliyotolewa na familia hiyo kama zawadi kwa yeyote atakayetoa taarifa za kupatikana kwa Mo.

 

MO amefikisha siku ya nane tangu kutekwa kwake huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi na kutoa taarifa za awali.

VIDEO: MSIKIE HAPA SIRRO AKIZUNGUMZA

Comments are closed.