The House of Favourite Newspapers

Sukari Kaa la Moto kwa Wafanyabiashara  

0

DAR: Licha ya kuwa ni bidhaa adimu yenye matumizi mengi kwa binadamu katika maisha ya kila siku, sukari imeendelea kuwa kaa la moto kwa wafanyabiashara, wananchi (watumiaji) na serikali kwa ujumla, IJUMAA linachambua.

 

Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba, bidhaa hiyo adimu imepanda kutoka Sh1,800 kwa kilo moja mwaka 2016 hadi Sh 4500 kilo moja kwa mwaka 2020 katika baadhi ya maeneo nchini.

 

Hata hivyo, bei elekezi mwaka 2016 ilikuwa Sh 1800 kwa kilo moja lakini sasa (2020) Serikali imetangaza kuwa bei elekezi ni Sh 2,600 katika baadhi ya maeneo hususani Dar es Salaam na Morogoro.

 

Hali hiyo imesababisha kuibuka kwa mtafaruku kati ya wafanyabiashara na serikali baada ya sukari kuadimika katika baadhi ya maeneo na bidhaa hiyo kupanda kutoka 2600 kwa kilo moja hadi kufikia Sh 4500 kwa kilo.

 

Aprili 24 mwaka huu Waziri wa Kilimo; Japhet Hasunga, alitangaza bei elekezi ya sukari kwa kila mkoa nchini, huku akiwaonya watakaobainika kuuza kinyume cha utaratibu huo kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kunyang’anywa leseni ya biashara.

 

Kutokana na kupandishwa kwa bei ya bidhaa hiyo kiholela, Hasunga alisema serikali imechukua hatua hiyo ili kudhibiti hali hiyo.

 

“Sheria ya Sukari Na. 26 ya Mwaka 2001 chini ya kifungu cha 11A, inampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya kilimo kutangaza bei ya ukomo wa juu ya sukari,” alisema.

 

Waziri huyo alibainisha bei kwa kila mkoa kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam (Sh. 2,600), Iringa, Njombe, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Singida, Tabora na Dodoma (Sh. 2,900), Lindi na Mtwara (Sh. 2,800), Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Tanga na Morogoro (Sh. 2,700).

 

Pia, mikoa ya Songwe, Mbeya, Mara, Kagera, (Sh. 3,000), Rukwa, Katavi, Ruvuma na Kigoma (Sh. 3,200).

 

WAFANYABIASHARA WALIA HASARA

Aidha, baadhi ya wafanyabiashara rejareja waliozungumza na IJUMAA walieleza kuwa, ni ngumu kwao kushusha bei ya bidhaa hiyo haraka kama serikali ilivyoagiza kwa kuwa walinunua kwa bei kubwa.

“Mfano mimi jumla nilinunua kilo moja Sh 3000 sasa nitauzaje 2,600? Hili ni jambo ambalo haliwezekani, wangewabana wale wauzaji wakubwa.

 

“Sisi wafanyabiashara wadogo wanatuonea kwa sababu hatutaweza kumudu gharama za uendeshaji kama tukipata hasara, hii sio fair kabisa,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao katika eneo la Mbezi.

 

Hali hiyo imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamekaidi agizo la kushusha bei ya sukari, hali inayoilazimu serikali kuchukua hatua.

Baadhi ya maeneo tayari sukari zilizokuwa zimehodhiwa na wafanyabiashara wakubwa, zimekamatwa na nyingine kutaifishwa huku baadhi ya wafanyabiashara wadogo nao wakikamatwa.

 

BODI, WACHUMI: WAFANYABIASHARA WAKUBALI HASARA

Licha ya kutangazwa kwa bei hizo elekezi, Mhadhiri wa masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humprey Moshi alisema lazima wafanyabiashara hao wakubali hasara, kuliko kuendelea kuwaumiza wananchi.

 

“Mbona mtu alikuwa na stock ya bidhaa zake, bei ikipanda na yeye anapandisha? Kuna siku watapata faida na siku watapata hasara, ukitangaza bei mpya ni mpya, ukiwaruhusu kuendelea kuuza stock waliyonayo kwa sababu walinunua kwa bei ya juu, itaendelea kuathiri wananchi.

 

“Naamini wafanyabiashara hawawezi kupata hasara, wanatake advantage ya hii Corona, kwa sababu watu wanafanya manunuzi ya jumla kujilinda na Corona, huu ni ujanja wa wafanyabiashara kutaka kutumia huu ugonjwa na ramadhani,” alisema.

 

Aidha, alisema waagizaji wa sukari wanajulikana na wakati wa kusafisha viwanda hao waagizaji ndio haohao wanaohodhi.

 

“Kwa hiyo, sio sahihi kufanya operesheni kwenye maduka, waende kwa hao wafanyabiashara wakubwa waliopewa leseni za kuagiza sukari. Kama wanafanya ujanja wafungiwe, wasiwabembeleze.

“Ni wakati wa serikali kuwa wakali zaidi, iwape adhabu inayouma kama uhujumu uchumi, akishikwa hatarudia tena,” alisema.

 

SBT WAPIGILIA MSUMARI

Akizungumza na IJUMAA, Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari nchini (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, alisema hakuna utaratibu dhidi ya wafanyabiashara hao wanaolalamika zaidi ya kuwakamata.

Alisema serikali ikitoa maelekezo, hakuna kingine zaidi ya kufuata, hivyo wanapaswa kuuza kwa bei elekezi iliyotolewa.

 

“Tunakamata wote na operesheni inaendelea, vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya msako huo,” alisema.

Alisema wafanyabiashara hao wakubwa na wadogo wanapokamatwa, hatua zinazofuata ni kuwapeleka mahakamani.

 

“Taratibu zipo. Siwezi kusema kwa makosa gani, ila sheria itatafsiri kulingana na kosa husika, kama aliyenunua sukari nyingi akaficha, huo ni uhujumu uchumi, kwa hiyo itategemea na kosa lake,” alisema.

Alisema mwaka 2019 hapakuwapo na mfumko wa bei kwa sababu bodi hiyo ilifanikiwa kudhibiti wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

 

SABABU ZA BEI YA SUKARI KUPANDA

Aidha, Prof. Bengesi alisema sababu za kupanda kwa bei ya sukari hutofautiana kila mwaka kulingana na historia yake.

Alitolea mfano kuwa mwaka huu ni kwamba, kama ilivyodesturi kila inapofika mwezi wa Machi hadi Aprili, viwanda husimamisha uzalishaji.

 

“Kwa hiyo, wafanyabiashara wanahisi uzalishaji ukisimama kutatokea upungufu mkubwa kwa sababu ni kweli nchi yetu huagiza bidhaa hiyo nje.

“Serikali kupitia bodi ya sukari huwa tunatoa vibali kuagiza nje, sasa vibali vikitoka ile sukari kama haijasarifishwa kuletwa nchini, wafanyabiashara wasio waadilifu wanaweza kuficha sukari na kuonesha kuna upungufu.

 

“Mwaka huu tulikuwa tunalidhibiti kama mwaka jana, ila wakati tunaingia kwenye kufunga msimu, kukatokea tatizo la Corona, nchi wasambazaji wa sukari wakawa wamefunga mipaka, watu hawafanyi kazi.

 

“Makampuni waliopata vibali vya kuingiza sukari, yalishindwa kupata mikataba kwa sababu mipaka ilikuwa tayari imefungwa. Kwa hiyo, wafanyabiashara wa ndani wakahodhi yaani wananunua wanaficha.

“Kwa hiyo, wanaachia kidogo kwa kudhani hakuna sukari itaingia kutoka nje, ila sasa sukari imeshaingia, hakuna upungufu. Baada ya wiki mbili bei zitakuwa level, baadhi ya sehemu zimeshashuka,” alisema.

 

HALI YA UZALISHAJI NCHINI

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, uzalishaji sukari ya kawaida nchini kwa mwaka ni tani 360,000.

“Mahitaji ya sukari kwa matumizi ya kawaida ni tani 470,000. Hivyo uzalishaji sukari ndani ya nchi umefikia 77% ya mahitaji ya nchi yetu. Ongezeko la 2.5% kwa mwaka. TZ inatarajia kujitosheleza na kuwa na ziada kufika 2024/25.

 

TATHMINI BEI YA SUKARI 2016-2020

Mwaka 2020 bei ya sukari imepanda kutoka 2600 hadi 4500 licha ya serikali kutangaza bei elekezi, baadhi ya wafanyabiashara hawajatekeleza agizo hilo.

Mwaka 2019 hapakutokea uhaba wa sukari kama ilivyokuwa mwaka 2018, hivyo bei ya sukari ilibaki kuwa kati ya 2300 hadi 2800.

 

Mwaka 2018, kulitokea uhaba mkubwa wa sukari na mafuta, ambapo bei ya sukari ilipanda kutoka 1800 hadi 3000.

Mwaka 2017 bei ya rejareja ya sukari ilikuwa kati ya Sh 2,600 na 3000, awali ilikuwa 1900 na 2200.

Mwaka 2016 Bodi ya Sukari (SBT) ilitangaza kushusha bei ya sukari kutoka Sh 2,000 hadi Sh 1,800 lakini wafanyabiashara walikuwa wanauza hadi Sh 2,500.

Stori: GABRIEL MUNSHI, Ijumaa

Leave A Reply