The House of Favourite Newspapers

Tambwe: Naijua Simba, Lazima Ianguke

Said Ally | CHAMPIONI| Dar es Salaam

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, raia wa Burundi, ameweka bayana kwamba utitiri wa michezo ya ugenini waliyonayo wapinzani wao, Simba, ndiyo itakuwa sababu kwa klabu hiyo kushindwa kutwaa ubingwa kwa msimu huu.

Tambwe, mwenye mabao tisa kwenye ligi, ameyasema hayo wakati kikosi cha Simba kinachonolewa na Joseph Omog raia wa Cameroon jana Jumapili kilianza harakati zake za kucheza michezo mitatu wakiwa ugenini kwa kuvaana na Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Mshambuliaji huyo ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kwa jinsi anavyoifahamu Simba, haitaweza kucheza mechi zake zote tatu ugenini bila kupoteza hata moja kutokana na kikosi hicho kuwa na wachezaji wengi ambao wanacheza vizuri wakiwa katika viwanja vizuri kama Taifa, Dar ambapo wamepazoea.

“Naamini kwamba tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kwa sababu Simba ninayoijua mimi ni lazima itaangusha pointi kwenye mechi zake tatu za mikoani, yaani kama watashinda basi mbili na moja lazima wafungwe au sare.

“Wale kikosi chao kinapata matokeo mazuri wakiwa nyumbani hapa Taifa kwa sababu wameshazoea kucheza katika mazingira mazuri sasa kule mikoani viwanja si vizuri tofauti na sehemu waliyozoea, sasa hilo naamini kwamba litakuwa tatizo kwao.

“Kama watapoteza pointi tu hiyo itakuwa faida kwetu kwa sababu tuna mechi moja pekee ya ugenini dhidi ya Mbao na tutatumia vizuri nafasi hiyo kuhakikisha kwamba tunatetea ubingwa wetu kwa mara nyingine tena,” alisema Tambwe.

Subscribe kwenye YouTube Chanel yetu ya Global TV Online ili zote kali zinazotufikia iwe nisiasa, michezo, comedy, burudani, stori za mastaa, muziki na nyingine zikufikie kwa wakati.

Comments are closed.