The House of Favourite Newspapers

Tanzia: Muigizaji Maarufu Mzee Mathiokore Afariki Dunia

0

ALIYEKUWA muigizaji nguli  na maarufu katika kipindi cha Gumbaru School kilichokuwa kipeperushwa kwenye Runinga ya K24 ya nchini Kenya, Mzee Mathiokore ‘Old Boy’, ameaga dunia. Kifo chake kimethibitishwa na produsa na mkurugenzi wake Kimathi Iceberg.

 

Mathiokore alipata umaarufu baada ya kuigiza katika vipindi kadhaa ikiwemo mashtaka na vingine vya lugha ya Kikuyu.

Kifo cha Mathiokore ambaye aliigiza katika vipindi vya Mashtaka, Ngumbaru na vinginevyo kilitangazwa na produza wake Kimathi Iceberg ambaye alisema tasnia ya uigizaji na sanaa kwa jumla imepata pigo kubwa sana na imempoteza mtu muhimu sana katika sanaa ya maigizo Afrika Mashariki.

 

Kimathi alisema alifanya kazi na Mzee Mathiokore hadi dakika ya mwisho lakini hivi maajuzi wakiwa naye mjini Meru, alionekana mdhaifu sana.

“Miezi minne iliyopita, tulienda Meru kushoot video flani na tuliporudi, mzee alionekana mnyonge na mdhaifu sana ila hakuwa mgonjwa, nimesikia tu kifo chake asubuhi ya leo (jana). Mzee huyu alikuwa akijituma sana kwenye tasnia pengine kuliko hata vijana,” Alisema Kimathi.

 

“Alikuwa mzee mzuri sana, nakumbuka shoo yake aliyofanya ya kwanza ilivutia sana, alikuwa mtu mwenye bidii, tulifanya pamoja miradi mingi, alikuwa na talanta ila tu aliingia katika sekta ya uigizaji kama umri wake umesonga, hata hivyo tunashukuru muda tuliyokuwa naye,” alisema Kimathi.

Leave A Reply