The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness -13

0

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake.

Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango.

Taratibu maisha ya Mashango yanaanza kubadilika kutokana na uwepo wa mtoto huyo, anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Upande wa pili, Hans na mkewe wanatumia vibaya mali za marehemu na kusababisha mahakama iingilie kati.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO

…Mahakama iliwapa agizo Hans na mkewe kwamba wanatakiwa kukabidhi kila kitu walichokabidhiwa na familia walipoteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi.

“Mungu wangu,” alisema Hans huku akimkodolea macho mkewe kwani kiukweli japokuwa haukuwa umepita muda mrefu tangu walipokabidhiwa kazi hiyo, tayari walishatumia kiwango kikubwa cha fedha zilizokuwa benki pamoja na zilizokuwa zinaingia kupitia miradi yao mbalimbali, kwa matumizi yasiyohusiana kabisa na malezi ya mtoto Arianna.

“Lakini nilikuwa nakwambia mume wangu, sema ubishi wako tu.”
“Mke wangu huu siyo muda wa kulaumiana tena, ujue naenda kufungwa mumeo,” alisema Hans kwa sauti ya chini huku akitetemeka, alishindwa kabisa kuificha hofu iliyokuwa ndani ya moyo wake.

Harakaharaka wakaondoka kwenye ofisi za mahakama hiyo na kurudi nyumbani kwao huku kila mmoja akionesha kuwa na mawazo mengi ndani ya kichwa chake. Hakuwahi kutegemea kama ndugu zake wanaweza kuchukua uamuzi mgumu kama huo.

Mara kwa mara walipokuwa wakimuita kwenye vikao vya ukoo na kumuonya kuhusu matumizi mabaya ya fedha za mirathi alizopewa kusimamia, alikuwa akiwapuuza kwani alijua hawawezi kumfanya chochote kwa sababu tayari alishapewa mamlaka na mahakama.

Uamuzi ambao ndugu zake waliuchukua hakuwahi kuutegemea hata siku moja, akawa anaumiza kichwa juu ya nini cha kufanya ili kuinusuru nafsi yake kwani kulikuwa na kila ishara kwamba jela ilikuwa ikimuita.
“Mke wangu.”
“Abee mume wangu.”

“Nimepata wazo.”
“Wazo gani mume wangu.”
“Unajua tukiendelea kubaki hapa, mimi nitafungwa na wewe na wanangu mtarejea kwenye maisha yaleyale ya umaskini, tena safari hii umaskini utazidi zaidi kwa sababu hamtakuwa na mtu wa kuwasaidia.”

“Unachokisema ni kweli mume wangu, mimi nahisi hata kuchanganyikiwa maana nauona ugumu unaokuja mbele yetu. Sasa umeamuaje?”

“Nimeamua kuchukua uamuzi mgumu. Nataka wewe na wanangu muanze kujiandaa. Tunaondoka usiku wa leo na usimwambie mtu yeyote kuhusu mpango huu.”
“Vipi kuhusu Arianna? Tunaondoka naye?”

“Hapana, huyo tutamuacha hapahapa kwenye huu mjumba alioachiwa na wazazi wake.”
“Sasa tunaenda wapi mume wangu na tutapata wapi fedha za kutuwezesha kuishi vizuri huko tunakokwenda?”

“Kuhusu mahali tunakokwenda hilo niachie mimi. Kuhusu fedha inabidi sasa hivi mimi nikamalizie kutoa pesa zote benki pamoja na kuuza vitu vyote ambavyo vinaweza kuuzika kwa urahisi, hapa hapatufai tena,” alisema Hans huku akitweta kutokana na hofu iliyokuwa imeutawala moyo wake.
“Hawawezi kutukamata mume wangu?”

“Hatuna namna mke wangu, ni bora wakatukamatie mbele kuliko kukaa hapa kama vifaranga vya kuku mbele ya kundi la mwewe.”
***
“Mama.”
“Abee mwanangu.”
“Hivi kwa nini mimi siendi shuleni kama wenzangu?”
“Mh! Mwanangu, kwa nini umeniuliza hivyo?”
“Naona watoto wenzangu wote wanasoma.”
“Na wewe unataka kusoma?”

“Ndiyo mama, nataka nikiwa mkubwa nikusaidie, nataka kuja kuwa daktari bingwa.”
“Mh! Na mimi napenda usome mwanangu lakini naogopa kukupoteza. Kuna watu wengi ambao hawatutakii mema, wanaweza kukudhuru mwanangu.”

“Lakini mama, sasa hivi mimi naweza kujilinda, isitoshe unaweza kuwa unakuja kunichukua shuleni mama, nataka kujua kusoma na kuandika kama wenzangu,” alisema mtoto mdogo Brianna lakini alipoona mama yake anakuwa mgumu kumkubalia, ilibidi aanze kuangua kilio kwani ni kweli alikuwa akijisikia vibaya sana anapowaona watoto wenye umri kama wake wakitoka shuleni wakati yeye akiwa mitaani na mama yake wakifanya biashara ndogondogo.

Kwa jinsi Mashango alivyokuwa anampenda mwanaye huyo, hakuwa tayari kumuona analia au anaumizwa na kitu chochote.

Japokuwa alikuwa anampenda mno na alikuwa na wasiwasi kwamba anaweza kupatwa na jambo baya akiwa mbali naye, aliamua kumruhusu kwa shingo upande kwani hakupenda kumuona akilia.
“Basi usilie mwanangu, nyamaza mama,” alisema Mashango na kumkumbatia Brianna, akamwambia asiwe na wasiwasi ataanza kufuatilia taratibu za kumuandikisha kwenye shule ya awali iliyokuwa karibu nao lakini akamsisitiza kuwa akianza shule awe makini na watu wenye nia mbaya.

Siku hiyo ilipita, kesho yake, Mashango aliwahi kuamka na kwenda kutafuta biashara kama kawaida akiwa na mwanaye, baada ya kupata mbogamboga na matunda ya kutosha kwa biashara ya siku nzima, walipitia pamoja kwenye Shule ya Msingi Mathare.

Kitendo cha mwanamke huyo kuonekana tu kwenye mazingira ya shule, kilisababisha wanafunzi waliokuwa madarasani kuanza kupiga kelele za kushangilia na kumuita jina lake kwani kipindi ukichaa wake ulipokuwa umekolea, alikuwa akisumbuana sana na watoto mitaani waliokuwa wakimuimba na kumfuata nyuma kwa makundi.

“Mashango! Mashango! Mashango! Kichaa! Kichaa!” wanafunzi walisikika wakipiga kelele kwa nguvu. Ilibidi walimu watumie nguvu za ziada kuwatuliza kwani wengine walishaanza kutoka kwenye madarasa yao na kumkimbilia. Hatimaye hali ilitulia, mtoto Brianna akawa amepigwa na butwaa akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea.

“Mama! Kwa nini wanakuimba na kukuita kichaa?” Brianna alimuuliza mama yake swali lililosababisha ashindwe kuzificha hisia zake, machozi yakawa yanamlengalenga. Alishindwa cha kumjibu zaidi ya kumshika mkono na kuanza kutembea naye kuelekea kwenye ofisi za mwalimu mkuu.

Leave A Reply