The House of Favourite Newspapers

Tizi la Pluijm Singida United, Wahenga Kazi Wanayo

0
Wachezaji wa Singida United wakiendelea na mazoezi.

 

KOCHA Mkuu wa Singida United, Hans van Der Pluijm hataki utani katika kuiandaa timu yake kwani amekuwa akiwafanyisha mazoezi ya kiufundi zaidi wachezaji wake kabla ya kuanza kwa msimu ujao.

Timu hiyo ambayo imepiga kambi hapa jijini Mwanza, jana Alhamisi asubuhi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nyamagana ambapo yalihudhuriwa na mashabiki kadhaa wapenda soka.

Katika mazoezi hayo yaliyoanza saa 1:30 asubuhi na kumalizika saa 3:30 asubuhi, mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo walikuwa wakisema “Kwa tizi hili, hao wakongwe ‘Wahenga’ Simba na Yanga lazima watakalishwa”.

Kocha Mkuu wa Singida United, Hans van Der Pluijm akiwa ma wachezaji wake.

Championi Ijumaa ambalo lilikuwepo katika mazoezi hayo, lilimshuhudia Pluijm akianza programu zake kwa kuwaambia vijana wake wazunguke uwanja kwa kukimbia taratibu, kisha wakanyoosha viungo ambapo walitumia dakika 30.

Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, akawabadilishia zoezi, safari hii akawaachia wachezaji wachezee mpira, kisha kupigiana pasi ndefu, fupi pamoja na kukokota mpira ambapo alikuwa makini kwa yule ambaye hajaelewa anamuelekeza jambo ambalo lilifanya muda mfupi kila mchezaji kuelewa nini kocha anataka.

Ilipofika saa 2:40, akawapanga vijana wake kwa mafungu manne, mabeki, mawinga, viungo na washambuliaji, kisha likaanza zoezi la kutengeneza nafasi za kufunga.

Wachezaji wakinywa maji.

Katika mabeki, waliongozwa na Elisha Muroiwa, kwenye kiungo kiongozi alikuwa Nizar Khalfan. Katika mawinga waliokuwa wakipiga krosi, waliongozwa na Shafik Batambuze, huku Danny Usengimana akiwaongoza washambuliaji.

Zoezi hilo lililochukua dakika 20, lilimpa sifa kubwa Usengimana kwani alionekana kujua nini anatakiwa kufanya kwa wakati gani kutokana na kwamba muda mwingi alikuwa akijitenga sehemu sahihi na kufunga mabao kirahisi.

Pluijm hakuishia hapo, aliwapa vijana wake wote mtihani wa kila mmoja kupiga mpira uende kugonga mlingoti wa juu wa goli bila ya kuwepo kwa kipa.

Zoezi hilo lilichukua dakika 30 ambapo wachezaji wote walitimiza jambo hilo. Baada ya hapo, Pluijm akasema kwa kifupi: “Nataka kuifanya timu hii kuwa ya kimataifa zaidi.”

 Stori: Omary Mdose | Championi Ijumaa

 

 

Leave A Reply