The House of Favourite Newspapers

Tuhuma za Rushwa! Askari Polisi 4 Wafukuzwa Kazi

0

ASKARI wanne wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha wamefukuzwa kazi na maofisa wawili wa Jeshi hilo wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni 100.

 

Taarifa hiyo imetolewa leo April 29, 2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, na kubainisha kuwa walipokea taarifa kuhusu askari hao mnamo Aprili 19, 2021 kuwa wameomba na kupokea rushwa ndipo uchunguzi ukaanza kufanyika.

 

“Baada ya uchunguzi Jeshi limewafukuza kazi askari wanne na kuwasimamisha kazi maofisa wawili kwa kuwa haliwezi kuvumilia tuhuma kama hizi,” amesema Masejo.

 

Amebainisha kuwa baada ya uamuzi huo hatua nyingine za kisheria zinafanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

 

Masejo amesema Askari hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa Profesa Justine Maeda ambaye amewahi kuwa mshauri wa uchumi wa Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Julius Nyerere. Wanadaiwa kuomba fedha hizo na kupatiwa baada ya kumpekua nyumbani kwake na kudai kukuta vipande viwili vya meno ya tembo vikiwa kwenye mzinga wa nyuki.

 

Profesa Maeda ameeleza kuwa alitoa fedha hizo ili ajinusuru asifunguliwe kesi ya uhujumu uchumi kama alivyoelezwa na polisi hao.

Leave A Reply