The House of Favourite Newspapers

Tundu Lissu Arejea Tanzania Baada ya Kupona

0

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) – Bara, Tundu Lissu, amewasili nchini baada ya kuwa ughaibuni kwa matibabu kwa takribani miaka mitatu, kufuatia shambulio la risasi akiwa Dodoma.

Lissu amewasili nchini  leo Jumatatu, Julai 27, 2020, majira ya saa 7 mchana akitokea Ubelgiji kwa ndege ya Shirika la Ethiopia na kupokelewa na viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa chama hicho katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

 

Baada ya kuwasili, umati ya watu waliojitokeza kumpokea mwanasiasa huyo, umeanza msafara kutoka uwanjani hapo kwenda Ofisi za Makamu Makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kutoka ndani akiwa ameongozana na viongozi wa Chadema akiwemo Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho na Katibu Mkuu wake, John Mnyika, shangwe zilitawala uwanjani hapo.

Lissu amerejea nchini mwake ikiwa ni takribani miaka mitatu tangu alipokuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi zaidi ya 30. Tukio hilo lilitokea mchana wa Septemba 7, 2017 katika makazi yake Area D jijini Dodoma na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa matibabu.

Usiku huohuo alisafirishwa akiwa hajitambui kwenda Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi hadi  Januari 6, 2018 alipohamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

 

Leave A Reply