The House of Favourite Newspapers

Tuzo Yataka Kumtoa Roho Nandy

0

 

UKIZUNGUMZIA wanamuziki wa kike wenye nguvu ndani ya Bongo Fleva kwa sasa, jina la Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, haliwezi kukosekana.

Hii ni kutokana na kipaji kikubwa alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu cha kuimba kwa umahiri kiasi ambacho mashabiki walimaliza bando zao za kutosha kumpigia kura hili anyakue Tuzo ya AFRIMMA zilizofanyika nchini Marekani hivi karibuni.

 

Taarifa ya kuwa mmoja wa wanamuziki watatu kutoka nchini Tanzania na Afrika Mashariki kupata tuzo hizo zilimshtua mno Nandy, kiasi ambacho mshtuko alioupata ulitaka kuitoa roho yake kwani ni kitu ambacho hakufikiria kama atashinda.

 

Nandy ametwaa Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike Afrika Mashariki huku Diamond akinyakuwa Mwanamuziki Bora wa Kiume Afrika Mashariki, wakati Zuchu yeye ametwaa Tuzo ya Mwanamuziki Chipukizi Afrika.

Nandy amefunguka mengi katika mahojiano maalum (exclusive interview) na Gazeti la IJUMAA, tiririka naye;

IJUMAA: Mambo vipi Nandy?

 

Nandy: Poa kabisa, vipi hali?

IJUMAA: Salama kabisa, hongera sana kwa tuzo.

NANDY: Asante sana, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu.

IJUMAA: Umejisikiaje kutwaa tuzo kubwa kama hiyo?

 

NANDY: Kwa kweli nilichanganyikiwa, sikuamini kwa sababu hata mimi sikuwaza kabisa kama nitachukua tuzo hiyo kwa kweli, maana hata nilipoambiwa nimeshinda, nusu roho initoke kwa furaha na kuchanganyikiwa kuwa ni mimi kweli.

IJUMAA: Kwenye tuzo hizo kubwa mmeshinda Watanzania watatu, wewe, Diamond na Zuchu, je, kwa vile wanawake kutoka Tanzania ni wawili tu, je, uslishawahi kumpigia simu

 Zuchu kupongezana au hata kufikiria kufanya naye kazi ya pamoja?

NANDY: Kuhusu kupigiana simu, hapana, hatujafanya hivyo, ingawa ninampongeza na yeye, lakini kuhusu kufanya kazi ya pamoja, wanaopanga hivyo ni menejimenti, siku wakipanga tufanye itakuwa sawa tu.

 

 

IJUMAA: Ni vigezo gani vimetumika katika mchakato mzima wa kupiga kura hadi kupatikana kwa mshindi?

NANDY: Ilikuwa ni kupiga kura tu, hivyo watu wamejitahidi sana kunipigia kura hadi nimeshinda maana hivyohivyo siyo rahisi kabisa na ndiyo maana nilishtuka sana.

 

IJUMAA: Ushindi wako ni ushindi pia wa mchumba wako, Billnass, amesemaje baada ya kusikia umeshinda tuzo hiyo?

NANDY: Kwa kweli amefurahi sana, tena sana kwa sababu mara nyingi anapenda kunitia moyo kwa kila jambo hata pale nilipotaka kukata tamaa. IJUMAA: Nimedhani na ndoa unataka kupigwa fastafasta kwa ajili ya furaha ya tuzo…

NANDY: Ndoa ipo tu hata kama hakuna tuzo, yule ni wangu na mimi ni wake imeandikwa tayari.

IJUMAA: Kuna Ngoma ya Nibakishie umeachia na King Kiba na inakimbiza mno, je, ni nani aliyeanza kumtafuta mwenzake ili mfanye kazi ya pamoja?

 

NANDY: Kila kitu kinafanywa na menejimenti yangu, lakini binafsi nimefurahi mno kufanya kazi ya pamoja na King Kiba. Kwangu ni fahari kubwa mno kwa sababu nilijua lazima utakuwa ni wimbo mzuri na utapendwa na kweli hicho ndicho kilichotokea.

IJUMAA: Billnass ni mchumba wako, unajisikiaje mnapofanya ngoma pamoja au unawezaje maana kuna uoga fulani unakuwepo, vipi kwa upande wako?

NANDY: Hapana, sina uoga wowote kwake kwa sababu tunajua sana kwenye muziki, hivyo tunapofanya ngoma ya pamoja tunavaa uhusika wetu vizuri mno na lazima ikubalike sokoni na kwa mashabiki wetu.

 

IJUMAA: Bado unaonekana kwenye Thamthiliya ya Huba, unawezaje kujigawa, muziki na sanaa ya uigizaji kwa wakati mmoja?

Nandy: Ninaweza kwa sababu zote ni sanaa na ni vitu ambavyo ninavipenda sana na vipo kwenye damu.

IJUMAA: Shukurani zako za dhati ziende kwa nani? NANDY: Mashabiki wangu ambao wamenipigia kura, uongozi wangu unaonisimamia na watu wote kwa pamoja.

Stori: Imelda Mtema

Leave A Reply