The House of Favourite Newspapers

Unaacha buku 2 unataka nyama?

0

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, bila shaka mu wazima, mnaendelea vema na ujenzi wa taifa letu, mimi namshukuru muumba kwani kila kukicha najiona mwenye furaha.

Kwa wagonjwa poleni, nawaombea dua Mungu awape uzima inshallah, leo nimeamua kuja na mada hii ya matumizi kwa sababu wanawake wengi wanaumia kuona waume zao wanawagombeza kwa sababu ya matumizi.

Unakuta mwanaume amemuachia mkewe shilingi 2,000 nyumbani, anaenda kazini na wana familia kubwa, akirudi anafunua chakula kama hajaridhishwa nacho utasikia akisema kuwa mbona umepika hiki, mimi leo sili.

Hivi mume unayefanya haya unafikiria nini labda nikuulize ingawa nitashindwa kupata majibu kwako kwa sababu hatuonani lakini ukijiuliza sana utapata majibu.

Mke unapomlaumu kila siku hajakupikia nyama unategemea atapata wapi hiyo nyama wakati hata hela unayomuachia kama matumizi haitoshi hata kununua nusu kilo ya nyama?

Wanawake wengi wanajikuta wameingia kwenye matatizo na waume zao kisa matumizi, sasa ushauri wangu kwako, wewe mwanaume mwenye tabia hiyo, nakusihi ufanye manunuzi yote mwenyewe, kisha weka kwenye friji au simamia kila kinachotoka, naamini utajua ni jinsi gani ulikuwa ukimuonea mkeo kwa kumdai ambacho hukumuachia.

Kama wewe ni mwanamke unayekutwa na adha hiyo, nakusihi usikubali kugombana na mumeo kwa sababu ya pesa, jaribu kukaa naye chini mpige mahesabu ya kile mnachotaka kula siku hiyo ili ajue anatakiwa kuacha shilingi ngapi.

Jenga tabia ya kumuuliza  mumeo kila siku atakula nini, siyo siku mojamoja, maana wanawake wakifurahi ndiyo huwa wanafanya hivyo,  ongea naye kwa unyenyekevu kabisa asijue sababu ya wewe kuamua kumuuliza, fanya kama ndiyo kawaida kabla hajatoka nyumbani kwenda kwenye mihangaiko, unamuuliza mume wangu leo nikupikie nini?

Hii itakata ugomvi wote kwa sababu kama atakuwa hana hela utampangia hela aliyonayo na ataondoka anajua kuwa kiasi alichoacha hakitoshi, mtajikuta mna amani tele na maisha yanaenda kama kawaida.

Wiki ijayo nitakuja na mada nyingine, mada hizi hutokana na malalamiko ya wasomaji wangu, hivyo msomaji kama wewe halijakutokea ni rahisi kumtokea mtu wako wa karibu.

Leave A Reply