The House of Favourite Newspapers

Urusi Yatishia Kuilipua Meli ya Marekani

0

SERIKALI ya Urusi imesema moja ya vikosi vyameli zake za kivita kimebaini kuwepo kwa meli nyingine ya kivita ya Marekani ambayo imeingia katika eneo la Urusi na kuanza kuifukuza meli ya Urusi katika Bahari ya Japan jana Jumanne.

 

Urusi imeshtumu meli hiyo ya Marekani ya USS John S McCain kwa kusafiri zaidi ya kilomita mbili kutoka eneo la mpaka na kusema ilitaka kuilipua meli hiyo. Baada ya kufukuzwa, meli hiyo ya kivita ya Marekani iliondoka eneo hilo, kulingana na taarifa kutoka Urusi.

 

Hata hivyo, jeshi la majini la Marekani limekanusha kufanya makosa yoyote na kusema meli yake “haijakatazwa” kufika eneo hilo.

 

Tukio hilo lilitokea Jumanne katika Bahari ya Japan, ambayo pia inafahamika kama Bahari ya Mashariki, eneo la maji linalopakana na Japan, Urusi na Korea zote mbili.

 

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Urusi, meli yake ya kivita ya Admiral Vinogradov iliwasiliana katika ngazi ya kimataifa kutoa onyo kwa meli za Marekani juu ya “uwezekano wa kuilipua meli husika kwa kuingia katika eneo lake la maji”.

 

“Taarifa ya Serikali ya Urusi ni ya uongo,” amesema msemaji wa jeshi la Marekani nchni Japan, Luteni Joe Keiley. “Meli ya USS John S McCain ‘haikukatazwa’ kuingia eneo hilo na taifa lolote lile.”

 

Msemaji huyo aliongeza kuwa Marekani haitatishika au kushinikizwa kukubali madai ya uongo kuhusu masuala ya majini kama yaliyotolewa na serikali ya Urusi.

 

Matukio kama hayo baharini ni nadra sana kutokea ingawa meli nyingine ya kivita ya Urusi ya Admiral Vinogradov iliwahi kuhusika na tukio la aina na meli ya kivita ya Marekani katika Bahari ya China Kusini mwaka jana. Nchi zote mbili Marekani na Urusi zililaumiana kwa tukio hilo.

 

Nchi hizo  mara nyingi hushutumiana kwa kuingiliana vibaya katika matukio ya kijeshi  iwe baharini au kwenye anga. Mwaka 1988, meli ya kivita ya Kisovieti ya Bezzavetny, iliikwaruza meli ya kivita ya Marekani ya Yorktown katika Bahari Nyeusi, kwa kuishutumu kwa kuingia kwenye eneo lake la maji.

 

Uhusiano kati ya Urusi na Marekani haujaimarika na Rais Vladimir Putin bado hajampongeza Rais Mteule, Joe Biden, kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Marekani uliofanyika Novemba 3 mwaka huu.

 

Nchi hizo  bado hazijakamilisha makubaliano ya mwisho ya silaha za nyuklia kati yao ambao utafikia ukomo wake Februari mwaka kesho. Mwaka 2017, meli hiyo ya kivita ya Marekani ya USS John S McCain ilihusika katika mgongano na meli ya mafuta ya Singapore, huku mabaharia 10 wakiuawa.

 

Leave A Reply