The House of Favourite Newspapers

Usijisahau, Tumia Kipindi Hiki Kujiandaa

0

wanafunzi1Kwanza niseme hongereni wanafunzi wote wa kidato cha nne ambao mmepitia kipindi kigumu cha mitihani yenu ya kumaliza elimu ya sekondari kwa levo ya kawaida yaani Ordinary Level.  Hii inaweza ikawa hatua kubwa sana kwa mtazamo wa wale walio chini yenu lakini kwa wakati huohuo hatua hiyo ikawa ndiyo kwanza mwanzo wa safari kwa wale ambao wamewapita kielimu; kwa maana ya wanafunzi wa vidato vya juu ‘Advanced Level, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata maprofesa na wanataaluma waliobobea kwenye fani fulani.

Mada yangu leo inawahusu wanafunzi hao waliomaliza na wengine wengi ambao katika vipindi fulani wamekuwa wakipumzika kwenye likizo zao na kujikuta wakisahau kabisa suala la kujisomea badala yake wakitamani kumaliza shule ili wapumzike na mzigo mzito wa kusoma.

Mfumo wa elimu yetu unamruhusu mwanafunzi apumzike aidha kwa likizo za kawaida au mapumziko ya kujiandaa kuingia levo nyingine ya masomo yake, hapa nazungumzia kipindi mara baada ya kumaliza darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na hata mara baada ya kumaliza elimu kwa ngazi ya chuo.

Ningependa ieleweke kuwa siyo jambo baya kwa mwanafunzi kutamani kumaliza haraka masomo yake ili apumzike. Kisaikolojia mtu yeyote akifanya kitu kwa muda mrefu huchoka na kutamani mapumziko, vivyo hivyo kwa mwanafunzi.

Hivyo basi suala hilo kama nilivyosema siyo baya kabisa, lakini tatizo huja pale ambapo mwanafunzi anafurahia uhuru anaoupata kwenye kipindi hicho cha mapumziko kiasi cha kusahau kujishughulisha na masuala yoyote yanayoendana na elimu hasa kusahau kujiandaa kwa levo nyingine ya elimu yake.

Mfano mwanafunzi anapokuwa likizo au anapomaliza levo moja ya elimu, kama anatarajia kuendelea na hatua nyingine na kuendeleza ufaulu wake anatakiwa ajiandae kielimu hasa kwa kupitia masomo ya awali kwa levo ya elimu anayotarajia kuingia mfano; masomo ya Pre-form One na Pre-form Five.

Mwanafunzi anayepitia masomo haya huwa mbali na kujiandaa kielimu pia hujiandaa kisaikolojia juu ya yale anayoenda kukutana nayo katika levo nyingine ya masomo yake ambapo hata kama hajafaulu, ari ya kusoma itamfanya arudie masomo aliyofeli au ajiendeleze kwa kozi nyingine ya masomo yake tofauti na yule ambaye katika kipindi hicho atakuwa amebweteka na kutofanya jitihada zozote ambapo atajikuta akiwa mgeni darasani na kuona kila kitu kigumu.

Leave A Reply