The House of Favourite Newspapers

Utajili wa Mondi UTATA WAIBUKA..

0

WAKATI jarida moja nchini Nigeria likimtaja msanii maarufu kutoka nchini Tanzania na katika Ukanda wa Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia thamani ya shilingi bilioni 11, utata mzito umeibuka juu ya umiliki wake wa Jengo la Wasafi Tower, Gazeti la IJUMAA linaripoti.

 

Hivi karibuni jarida hilo lilimtaja Diamond au Mondi kushika nafasi ya 28 katika ya orodha ya wasanii 30 wenye utajiri mkubwa waliorodheshwa huku akimpiku mkongwe wa muziki wa Lingala Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Le Grand Mopao Koffi Olomide; jambo lililosababisha baadhi ya mashabiki wa muziki kujadili uhalisia wa utajiri wake.

 

Mondi ambaye ndiye msanii wa Tanzania pekee aliyepenya kwenye orodha hiyo, aliibua mjadala mkali kuhusu utajiri na mali anazomiliki kwa jumla huku baadhi ya wachambuzi wa burudani wakitofautiana kwamba amepigwa kumbo na kushika namba za mkiani ilihali baadhi wakiona ameng’aa kuingia kwenye orodha hiyo hakuna msanii wa Tanzania liyewahi kutajwa kwenye orodha hiyo.

 

Wachambuzi hao walikwenda mbali zaidi akiwemo msanii mwenzake, Hamis Ramadhan ‘H Baba’ ambaye alilieleza Gazeti la IJUMAA kuwa, mali zilizothaminishwa katika ujenzi wa taswira ya utajiri wa Mondi ni za uongo; yaani ni kiini macho.

 

Alitolea mfano baadhi ya mali hizo ikiwemo Wasafi Tower ambalo ni jengo refu lililopo Mikocheni jijini Dar, kwamba licha ya Mondi kuanika kuwa limekamilika kwa asilimia 95, Novemba mwaka jana, hadi sasa hakuna kinachoendelea.

 

Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi, walipinga madai ya kutathmini mali zinazoonekana na kutangazwa kwa umma pekee ambapo walifafanua kuwa, utajiri wa Mondi au wa mtu yeyote pia hupimwa kulingana na nyaraka zilizopo benki na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja alisema kuwa, taasisi kama Forbes hufuatilia kwa makini miamala na pesa zilizohifadhiwa benki na hata nyaraka zinazopitia katika Mamlaka ya Mapato Tanzania –TRA.

 

Alisema kuwa, suala la kupima mali zinazoonekana si kigezo pekee cha kutathmini utajiri wa mtu.

 

FELA AVUNJA UKIMYA

Aidha, baada ya kuibuka utata kuhusu umiliki wa Mondi katika jengo hilo la Wasafi Tower, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na mmoja wa mameneja wa msanii huyo, Said Fela ‘Mkubwa Fela’ ambaye alivunja ukimya kuwa, jengo hilo ambalo licha ya kutangazwa kwa mbwembwe kwenye mitandao ya kijamii, hadi sasa hakuna kinachoendelea na kuibua maswali kwa mashabiki wake.

 

Fela alisema kuwa, mipango ya Wasafi Media kuhamia katika jengo hilo ambalo litakuwa makao makuu ya kampuni hiyo, bado ipo ila kinachosubiriwa kwa sasa ni Mondi ambaye alikuwa nchini Afrika Kusini.

 

“Mipango ya kuhamia makao makuu bado ipo, lakini Mondi mwenyewe atakuja kuzungumza kila kitu pindi atakaporejea kutoka Afrika Kusini,” alisema Fela kabla ya Mondi kutua Bongo juzi.

 

IJUMAA KAZINI

Baada ya kuzungumza na meneja Mkubwa Fela, Gazeti la IJUMAA lilifunga safari hadi kwenye jengo hilo refu na kufanikiwa kuzungumza na baadhi ya watu ambao walikiri Mondi kununua sehemu ya mjengo huo na siyo wote kama ambavyo watu wengi walikuwa wanafahamu.

 

“Ni kweli Mondi alikuja kununua hapa eneo kwa ajili ya kufanya iwe makao makuu ya Wasafi Media, lakini hajanunua jengo zima kama ambavyo watu wanadai, amenunua floo moja tu, hivyo akirudi kutoka Afrika Kusini ndiyo atakuja kupazindua rasmi,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mlinzi kwenye jengo hilo.

Stori: Memorise Richard, Dar

Leave A Reply