The House of Favourite Newspapers

Virusi vya Corona Vyazua Hofu kwa Mastaa Bongo

0

DAR: KUFUATIA mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na kirusi aina ya ‘Corona’ kuikumba nchi ya China na nchi nyingine duniani, baadhi ya mastaa nchini wakiwamo wasanii, wanamitindo na wafanyabiashara wameeleza hofu yao juu ya ugonjwa huo na kuapa kutoenda China hadi hali itakapotengemaa.

 

Ugonjwa huo umekuwa ukisambaa kwa kasi ambapo kumekuwa na ongezeko la wagonjwa pamoja na vifo katika kipindi kifupi kwa wastani wa zaidi ya wagonjwa 200 kwa siku.

 

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tangu mlipuko wa ugonjwa huu uanze katika mji wa Wuhan uliopo katika jimbo la Hubei nchini China Disemba, 2019 hadi 28 Januari, 2020 jumla ya watu 4,593 wamethibitishwa kuugua ugonjwa huo duniani kote, ambapo kati yao, vifo 106 vimetokea nchini China.

 

Aidha, ugonjwa huu umesambaa katika mataifa mengine 14 duniani yakiwemo Japan, Jamhuri ya Korea, Vietnam, Singapore, Australia, Malaysia, Cambodia, Thailand, Nepal, Sri Lanka, Marekani, Canada, Ufaransa na Ujerumani.

 

Vilevile kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika, walioripotiwa kuhisiwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo katika Bara la Afrika wanaendelea kufuatiliwa na kufanyiwa uchunguzi katika nchi za Ivory Cost, Ethiopia, Mauritius, Kenya na Zimbabwe.

 

MASTAA ROHO JUU

Baadhi ya mastaa nchini ambao walikuwa wakifanya safari zao nchini China mara kwa mara, wamezungumza na IJUMAA huku baadhi yao wakiapa kutokanyaga tena China.

 

JACQUELINE WOLPER

Staa huyu ambaye mara nyingi husafiri kueleka China kuchukua mizigo mbalimbali ikiwamo ya vitambaa nchini humo, amesema hafikirii tena kwenda huko na badala yake atakwenda kununua vitambaa Dubai.

 

“Yaani sijui niseme nini… kwenda huko mimi haiwezekani kabisa, nimeogopa sana! Sasa vitu vyangu vya ushonaji nitaenda kuchukulia Dubai, kule China siwezi tena, nimeogopa mno,” alisema Wolper.

 

KAJALA MASANJA

Msanii huyo amesema kuwa alikuwa anaipenda sana nchi hiyo na si mara yake ya kwanza kwenda China, lakini hawezi kwenda ingawa alikuwa amepanga kwenda Machi mwaka huu.

“Hapana, hata unipe kiasi gani cha fedha siwezi kwenda huko, nikisikia idadi ya waliokufa nachanganyikiwa,” alisema Kajala.

 

AUNT EZEKIEL

Ni mmoja wa mastaa ambaye naye alipanga kwenda kuchukua bidhaa zake za vipodozi nchini humo ili kufungua duka lake lakini ameamua kusitisha jambo hilo.

“Mimi siwezi kwenda tena, hivyo vipodozi vinisubirie tu sina mpango navyo kwa sasa kabisa. Bado naipenda familia yangu,” alisema Aunt.

 

SHAMSA FORD

Msanii huyo ambaye amefungua duka la kuuza madera, amesema ndoto kubwa ya mwaka huu ni kulipanua duka hilo na kuanza kufanya biashara nyingine ikiwemo nguo za aina mbalimbali.

“Yaani mwaka huu nilikuwa na mpango wa kwenda China lakini huwezi amini nimebadilisha maamuzi, nimeogopa na wala siwezi kwenda tena mpaka mwaka huu upite,” alisema.

 

IRENE UWOYA

Staa huyu ambaye si mpenzi sana wa kusafiri, amesema amewahi kwenda nchini China na mwaka huu alikuwa amepanga kwenda kutembea lakini kutokana na virusi hivyo vilivyoibuka, ameogopa kupanga safari hiyo tena.

“Ni ngumu sana kwangu kuwa na mawazo hayo na wala sihitaji kabisa, nina hofu kubwa mno,” alisema.

 

JANE RIMOY “SANCHI”

Mwanamitindo huyo alisema kuwa yuko mbioni kufungua duka lake la bidhaa za urembo lakini mzigo wote wa bidhaa hizo upo China jambo linalomchanganya akili.

“Unavyoniona nina mzigo wangu mkubwa wa duka langu na sijajua lini nitaufuata au kuukagua kwa sababu siwezi kufanya lolote kwa sasa,” alisema Sanchi.

 

JACQUELINE OBEID

“Mimi si unajua safari zangu za mara kwa mara ni China, sasa hivi nimetulia kabisa wala sina mzuka; hali ikiwa shwari nitaanza tena kwenda,” alisema.

 

SERIKALI YATAHADHARISHA

Aidha, Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Ummy Mwalimu, jana ametoa tahadhari kwa umma kuhusu ugonjwa huo aliofafanua kuwa unaambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na majimaji yenye virusi kutoka kwa mtu mmoja kwa njia ya kukohoa, kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa.

 

Alisema ingawa mpaka sasa Tanzania haina mgonjwa wala muhisiwa wa ugonjwa huo, wananchi wote wanashauriwa kuchukua hatua zifuatazo ili kujikinga nao:

“Kuzingatia kanuni za afya na usafi ikiwa ni pamoja na kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua mwenye historia ya kusafiri katika nchi zilizokumbwa na mlipuko au mwenye dalili zilizotajwa hapo juu.

 

“Kutokana na mwenendo na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo kipindi hiki cha mlipuko, Wizara inashauri kusubiri na kuepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri basi wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini.

 

“Kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo uliyovaa sehemu za mikono na kuepuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa,” alisema.

 

Pia aliongeza kuwa ni muhimu kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni na kuwahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili zilizoainishwa.

 

“Toa taarifa ya uwepo wa mtu mwenye dalili zinazohisiwa kuwa za ugonjwa huu kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu nawe au piga simu namba 0800110124 au 0800110125 bila malipo,” alisema.

Stori: Imelda Mtema, Ijumaa

Leave A Reply