The House of Favourite Newspapers

Diamond Alikoroga kwa Waislamu, Shehe Mkuu Dar Akereka, Atoa Tamko Zito…

Diamond Platnumz (kulia) akiwa na Babu Tale.

Na HAMIDA HASSAN| GAZETI LA IJUMAA| HABARI

DAR ES SALAAM: Msanii wa kiwango cha kimataifa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ hivi karibuni alijikuta akilikoroga kwa Waislamu baada ya kutupia mtandaoni vito mbalimbali vya madini ya dhahabu na almasi vilivyomo mwilini mwake kisha kujigamba kuwa ametumia kiasi cha shilingi 158,000,000.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar, Alhad Musa Salum.

Baada ya majigambo hayo, baadhi ya watu walianza kutupia comments zao, wengi wakimpongeza kwa mafanikio aliyopata lakini wengine wakahoji sababu za kutumia pesa nyingi kwenye vitu hivyo wakati kuna watu wenye shida wanaohitaji msaada wake.

 

“Ya nini utumie pesa nyingi hivyo kwenye vitu hivyo kaka, wapo watu wana shida, wanalala na njaa, wewe unatumia pesa zote hizo kwenye hiyo anasa, angalia jinsi ya kuwasaidia wenye uhitaji…” aliandika shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Twizzda1.

Baada ya shabiki huyo kuandika hivyo, ndipo zikaanza meseji ambazo zilikuwa zikimtaka msaniii huyo kuweka utaratibu mzuri wa kusaidia jamii ikiwa ni pamoja na kutoa sadaka.

 

Kufuatia wengi kuonesha kumshutumu kutotumia vizuri pesa zake kwa kuwasaidia watu wenye shida, akiwemo mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la kimtandao la @the_holyday, uzalendo ulimshinda Diamond na kuamua kufunguka mambo ambayo yalionesha kuwakoroga Waislamu.

Diamond aliandika hivi: @the_hoyday nimejenga nyumba 5 mwaka jana Iringa, misikiti miwili, mmoja Moro na pia mwingine Mtwara na madrasa Tegeta na nyumba ya imamu, sadaka mbalimbali, sasa unataka nitoe hela zote sadaka nami nisifurahishe nafsi yangu, hembu niombe radhi kwa hilo.

Baada ya kuandika maneno hayo, ndipo wadau mbalimbali, baadhi wakiwa ni waumini wa dini ya Kiislamu walipokorogwa na kuanza kueleza kuwa, anachokifanya Diamond siyo taratibu za dini yao.

“Miongoni mwa taratibu za Kiislamu katika kutoa sadaka, hutakiwi kuitangaza, inatakiwa ibaki siri yako na Mungu wako, unapotangaza kwamba umefanya hivi na vile unatarajia nini, hii siyo sawa Diamond…” aliandika mmoja wa wachangiaji.

Mwingine akaandika:

“Hapa ulipofikia siyo, unaanzaje kujitangaza hivyo, ni kweli umefanya mambo makubwa sana ambayo thawabu zake si ndogo, lakini unakwenda kinyume na taratibu za dini, ukishatangaza hivyo na watu wakajua umefanya yote hayo, lazima watakusifia lakini ujue kwa Mungu huna chako… huna chako kwa kuwa, si tayari umeshasifiwa duniani.”

Hata hivyo, mmoja aliyeonesha kuwa na busara ali-comment hivi:

Diamond, uliyofanya ni mambo makubwa sana, malipo yake si madogo na ndivyo inavyoshauriwa kwa wale waliojaaliwa kuwa nacho kutoa zaka na sadaka pale inapobidi, ulichokosea ni kujitamba mtandaoni, unaweza kutubu kwa hilo. Baada ya Waislamu wengi kutokwa na povu kufuatia kitendo cha Diamond kujitangaza mambo aliyoifanyia dini yake na hili la kuvaa vito vya bei mbaya,

Ijumaa lilimtafuta Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar, Alhad Musa Salum ambaye alisema:

“Kwanza kwa mtoto wa kiume kuvaa vitu hivyo ni haramu halafu hili la kujitangaza mambo aliyofanya itategemea amefanya hivyo kwa nia gani, kama nia ilikuwa kuwafanya watu wajue tu kafanya hayo ndani ya Uislamu, hiyo ni ria na ria siyo kitu kizuri hata kidogo. “Lakini pia anaweza kuwa amefanya hivyo ili kuwahamasisha wengine wafanye, hilo si tatizo. Kwa hiyo hapo itategemea na nia yake.”    

 

Comments are closed.