The House of Favourite Newspapers

Wananchi Wabuni Mbinu Mpya ya Kusajili Laini

0

DAR: WAKATI zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kumalizika kwa muda wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole, imebainika kuwa baadhi ya watu ambao hawajapata namba za Kitambulisho cha Taifa (NIDA), huwatumia ndugu, jamaa na marafiki waliopata namba hizo kusajili laini zao. IJUMAA linaripoti.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais John Magufuli kuagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini, (TCRA) kuongeza muda wa usajili kutoka Januari Mosi hadi Januari 20, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa wananchi ambao hawajasajili laini zao wasajili kabla ya kuzifungia.

 

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo Desemba 27 mwaka jana mara baada ya kusajili laini yake kwa alama za vidole akiwa mapumzikoni nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

 

Aidha, kwa mujibu wa uchunguzi wa IJUMAA, imebainika kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la ndugu na jamaa wenye namba hizo za vitambulisho, kubeba laini za ndugu zao kwenda kuwasajilia jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.

 

“Kuna binamu yangu amenipigia simu anaomba nikamsajilie laini, nimekataa maana akienda kufanya uhalifu huko, balaa litaniangukia mimi!,” alilalamika mmoja wa Mkazi wa Ilala aliyezungumza na gazeti hili.

 

Hata hivyo, baadhi ya vyanzo mbalimbali vimelieleza IJUMAA kuwa hata wanafunzi, watoto ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 kuruhusiwa kumiliki laini kwa mujibu wa sheria, nao wamekuwa wakitumia mbinu hiyo ya kuwaomba ndugu na jamaa waliofikisha umri huo kuwasajilia laini zao.

 

“Ni kwamba mtu kama ana laini ya mtandao mmoja, ndugu au rafiki yake hana kitambulisho, humuomba kumsajilia laini nyingine, hivyo mtu huyo kusajili mitandao miwili au mitatu lakini kwa watumiaji tofauti,” alisema mtoa habari wetu.

 

Watumia simu watakiwa kuchukua tahadhari

Kutokana na hali, hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa tahadhari kutokana na aina mbalimbali za uhalifu unaofanyika kwa njia ya simu, wanadhibiti uhalifu huo.

Taarifa hiyo ya polisi ilionya kuwa, “Usikubali kumsajilia mtu laini yake kwa jina lako hata kama mtu huyo ni wa karibu sana, kama baba, mama, dada au kaka.

 

“Kumbuka namba yako imesajiliwa, moja ya matukio ya kihalifu yakitokea na namba yako kuonekana, moja kwa moja unakuwa mtuhumiwa namba moja.

“Wengi wamepewa kesi za mauaji, wizi bila kujua, polisi wapo kazini wanapoona vidhibiti wanachukua kwani hawatojua kama umehusika au hujahusika.

 

“Usinunue simu za Android kwa mtu usiyemjua. Hiyo ni hatari kwani hujui hiyo simu imetolewa wapi, inawezekana ukapewa kesi ya wizi au mauaji endapo simu hiyo ilikuwa imeibiwa kwa mtu aliyeuawa, chukua tahadhari.

“Unapoiona laini ya simu njiani ipo chini usiiokote na kuiweka kwenye simu yako ili kujua ina salio kiasi gani na ujihamishie, ni hatari,” ilisema taarifa hiyo.

 

Pia TCRA imeonya kuhusu mbinu hiyo ambayo imeeleza kwamba ni kinyume cha sheria. Mmoja wa maofisa wa mamlaka hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandika jina lake kwa kuwa siyo msemaji, alisema atakayefanya kosa hilo akikamatwa atajikuta akiangukia katika mkondo wa sheria.

 

Hali ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole

Wakati hayo yakiendelea, takwimu zilizotolewa jana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonyesha hadi kufikia Januari 7, mwaka huu laini zilizokuwa zimesajiliwa ni milioni 25 sawa na asilimia 52.42 ya laini milioni 48.

 

Takwimu hizo zilizotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Frederick Ntobi zilibainisha kuwa bado laini zaidi ya milioni 20 hazijasajiliwa.

Usajili wa laini hizo umekumbwa na changamoto kubwa kutokana na wananchi kutokuwa na vitambulisho vya taifa au namba za utambulisho zinazotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

 

Baadhi ya wananchi waliozungumza na IJUMAA, walibainisha kuwa changamoto kubwa inayojitokeza ni uzembe unaosababishwa na maofisa wa Nida ikiwamo kushindwa kurekebisha makosa yanayojitokeza wakati wa upigaji picha.

 

“Mimi ni mkazi wa Kahama, nilienda kukata kitambulisho cha NIDA, nikafikia hatua ya kupiga picha, nikakaa zaidi ya wiki mbili kisha nikarudi, nikaambiwa picha haikutoka vizuri, nikapiga nyingine, nikakaa tena wiki kadhaa, narudi naambiwa taarifa zangu hazina fomu ya kiapo cha mzazi, hivyo nikalazimika kutoa Sh 10,000 ili nipate fomu hiyo (affidavit) kwa mawakili waliopo nje ya ofisi za Nida, hivyo unaona ni kwa namna gani tunapata shida,” alisema.

 

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi wanatahadharisha kuwa Serikali ipo hatarini kupoteza mapato kwa kuwa zaidi ya nusu ya laini za simu nchini hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa

Leave A Reply