The House of Favourite Newspapers

Warembo Hawa Walikimbiza Mbaya

0

GUMZO linaloendelea ni juu ya maisha ya mwanamama Pauline Zongo ambaye ni miongoni mwa warembo walioweka msingi wa mabinti kujiingiza kwenye muziki, lakini sasa anakabiliwa na changamoto za kiafya akidaiwa kujiingiza kwenye ulevi wa kupindukia na sasa anahitaji msaada wa kibinadamu akiwa sober house.

 

Pauline Zongo ameibua mjadala wa wasanii wa kike wa Bongo Fleva ambao walitamba katika uwanja huo na kujipatia sifa nyingi, lakini leo hawasikiki kabisa. Safu hii leo itakukumbusha wasanii hao;

PAULINE ZONGO

Pauline Zongo; huyu ni dada mwenye kujua kuimba kwa sauti tamu, lakini pia ana ujuzi wa kupiga gitaa, kinanda na ngoma.

Huyu alitamba akiwa katika Kundi la East Coast Team ambalo lilisheheni wasanii wakali kama AY, MwanaFA, King Crazy GK, O-Ten, Abbas, Snare na wengine.

 

Pauline Zongo alishiriki ngoma mbalimbali za kundi hilo na nyingine zikiwemo za kisiasa.

Msanii huyu alishirikishwa na Crazy GK katika ngoma mbalimbali kama vile Nitakufaje, Kosa Langu, Desire na Sister Sister.

 

Baada ya kung’ara katika uimbaji alichukuliwa na Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) iliyokuwa chini ya Kapteni John Komba na kumpa cheo cha kuongoza bendi hiyo.

 

Akiwa TOT, alitisha kwani alishiriki ngoma mbalimbali ikiwemo ya Mnyonge Mnyongeni aliyoimba kwa umahiri mkubwa kwa kushirikiana na waimbaji Abdul Misambano na Badi Bakule.

Hata hivyo, haikueleweka mkataba wake na bendi hiyo uliishaje, lakini mwaka 2018 akiwa anahojiwa, alisema aliahidi kuwa angerudi kwenye gemu.

HAFSA KAZINJA

Hafsa aliibuka kutokea BSS na alitamba miaka 13 iliyopita na Ngoma ya Pressure akimshirikisha Banana Zorro; ngoma iliyotamba kila kona, hakika alitisha.

Hata sasa katika YouTube ngoma hiyo ina watazamaji zaidi ya milioni moja. Hafsa sasa anaimba nyimbo za Injili kama Wewe ni Mfalme.

DATAZ

Ngoma iitwayo Wajua iliyoimbwa na Dataz akimshirikisha kaka yake, Squeezer ilikuwa moto wa kuotea mbali.

Dada huyu mwaka 2012 alipakua ngoma kali iitwayo Mume wa Mtu aliyomshirikisha msanii Joan ambayo ilitikisa na baada ya hapo, Dataz akapotea kwenye ramani ya muziki.

MAUNDA

Maunda Zorro, ni msichana anayetokea kwenye familia ya wanamuziki kuanzia kwa baba yake, Zahir Zorro na kaka yake, Banana Zorro; wote inaweza ikawa ni watu waliomfanya naye awe mwanamuziki.

Enzi zake alitesa na ngoma mbalimbali ikiwemo Nataka Niwe Wako aliyoipakua mwaka 2008, ukifuatiwa na Mapenzi ya Wawili aliyotoa mwaka 2009.

 

Pia msanii huyo alishirikishwa na wasanii mbalimbali akiwemo K-One kwenye Ngoma ya Yule, Squeezer kwenye Ngoma ya My Wife, Hussein Machozi kwenye Ngoma ya Hello na Nay wa Mitego kwenye Ngoma ya Talaka. Hakuna ubishi kwamba huyu alitisha.

RAH P

Huyu nilikuwa namfahamu sana enzi hizo kwani alikuwa akifika ofisini kwangu na kubadilishana mawazo na alitamba kwenye muziki wa kufokafoka (Hip Hop).

Ngoma yake ya Hayakuhusu ilitikisa anga za muziki Tanzania pia kabla ya hapo alishatoa ngoma kali iitwayo Malkia iliyokuwa ikizungumzia mateso mbalimbali anayopitia mwanamke.

 

Hata hivyo, Rah P alipotea ghafla kwenye gemu baada ya kwenda Marekani ambako huko alizaa watoto wawili na mwanaume ambaye alikamatwa kwa tuhuma za dawa za kulevya na kumuacha akiteseka na malezi.

SISTER P

Sister P alikuwa akishindanishwa sana enzi hizo za miaka 2000 na Zay B katika muziki. Alijulikana kwa ngoma zake kali kama vile Achana Nao aliyoimba na msanii wa muziki wa Dansi Bongo, Ali Choki ‘Kamarada’ au ‘Mzee wa Farasi’ aliyekuwa nyota na Kiongozi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ na Extra Bongo.

Alitunga ngoma nyingine kama Hey DJ na Nani Mkali akiwa na Nay wa Mitego.

ZAY B

Huyu kama nilivyoeleza hapo juu alikuwa mpinzani wa jadi wa Sister P. Ngoma iitwayo Niko Gado aliyoimba na Inspekta Haroun ndiyo iliyompa umaarufu mkubwa. Hata hivyo, baadaye aliimba ngoma nyingine nyingi kama vile Monica, Penzi la Teja akiwa na Rahima Kipozi wa Kundi la Unique Sisters na Haina Shobo; hakika alitesa mno kwenye muziki.

BESTA

Ni miaka miaka 14 sasa imepita tangu alipoachia ngoma aliyoiita Kati Yetu na ilikuwa moto mkali kutokana na ilivyopokelewa na Wabongo.

Huwezi kumtaja Besta bila kutaja Ngoma ya Dancehall aliyoitoa mwaka 2007 ambayo ilimfanya atambe hasa kwa staili yake ya kukata mauno iliyomfanya azidi kupendwa.

 

Mwaka 2011, Besta alifunga ndoa na msanii mwenzake mwimbaji Marlaw na kuanzia hapo hakuwa akionekana tena kwenye majukwaa ya muziki. Haijulikani kama alikatazwa au vipi.

 

Hakika wasanii hao wa kike wameacha swali kwani tunamuona Lady Jaydee tu sasa akiendeleza ngoma kwa upande wa Bongo Fleva kwani sasa ana miaka 21 kwenye gemu. Alianza na ngoma kali ya Machozi aliyoipakua mwaka 2000, hajachoka. Nawashauri wanawake wasanii niliowataja kumtafuta Komando Jide ili awape siri ya mafanikio yake kwenye gemu.

Makala: ELVAN STAMBULI, DAR

Leave A Reply