The House of Favourite Newspapers

Wasafi Festival vs Fiesta…. Vita si ya Kitoto

0

STAA wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na timu yake ya Tamasha la Wasafi na ile ya Tamasha la Fiesta, zinadaiwa kuingia kwenye vita ambayo siyo ya kitoto, Amani limedokezwa.

 

Baada ya Wasafi Festival kufikia fainali kwenye Viwanja vya Posta-Kijitonyama jijini Dar hivi karibuni, wikiendi hii ni zamu ya Fiesta kwenye Uwanja wa Uhuru.

 

KIBA, HARMO WAUNGANA

Kwenye Fiesta, mahasimu wawili wa Diamond au Mondi, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’ wameungana na kufanya vita hiyo kuwa nzito kutokana na wingi wa mashabiki wao.

 

Inaelezwa kuwa, Kiba na Harmonize au Harmo wamepania ile mbaya kuvunja rekodi inayoshikiliwa na Mondi ya kufanya shoo ya kibabe zaidi jijini Dar kwa mwaka huu aliyoiweka kwenye Wasafi Festival akiwa na mastaa kutoka Nigeria, Wizkid na Tiwa Savage.

 

HARMO KATIKATI YA MONDI NA KIBA

Amani linafahamu kwamba, kutoka kwenye ushindani wa Mondi na Kiba, katikati yao sasa yupo Harmo ambaye amekaa upande wa Kiba.

 

Watu wa karibu wa Kiba na Harmo, wanatamka waziwazi kwamba, wawili hao wamepanga kumaliza ufalme wa Mondi katika kufanya shoo kwani ‘watafia’ jukwaani usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu ya Sherehe za Uhuru, Desemba 9.

KIINGILIO KAMA FIMBO

Hata hivyo, suala la kiingilio kidogo cha shilingi elfu tatu linachukuliwa na Wasafi kama fimbo ya kuwachapia Fiesta.

 

Wanasema kwa kiingilio hicho, kuna wakati utafika kiingilio kitakuwa ni bia kama zinavyofanya bendi za muziki wa dansi kwa sasa.

 

Wanachojivunia Wasafi Festival ni kwamba wao walifanya kiingilio cha chini kuwa ni shilingi elfu 10 ambapo walipata zaidi ya watu elfu kumi.

 

Kwa upande wao, Fiesta wanaamini kwa kiingilio hicho wataujaza Uwanja wa Uhuru unaoingiza takriban watu elfu 20.

Hoja ya upande wa Fiesta ni kwamba, wameweka kiingilio kidogo kiasi hicho ili kila mtu awe na uwezo wa kuingia uwanjani hapo.

 

Sasa, Wasafi Festival wanadaiwa kutumia kigezo hicho kuonesha kwamba, Kiba na Harmo ni wasanii wa bei ndogo.

 

Mmoja wa viongozi wa Wasafi, Ricardo Momo anasema kifuatacho kwenye shoo hiyo (Fiesta) kiingilio kitakuwa ni bia.

“Mungu awaepushe isije kufikia kiingilio bia,” anasema Ricardo Momo.

 

MONDI KICHEKO

Kufuatia maoni hayo ya Ricardo Momo, Mondi alishindwa kujizuia na kujikuta akiachia kicheko kwa kutumia vikatuni (emojis) vinavyocheka.

 

SALLAM ARUSHA DONGO

Kwa upande wake mmoja wa mameneja wa Wasafi, Sallam SK alirusha dongo kuhusu Fiesta;

“Kiingilio 3,000 tiketi za awali, getini maelewano, uzalendo kwanza, Freesta, tudumishe upendo kwa wazee wetu wa kale. Kushusha bei nacho ni kipaji.”

 

BABU TALE NAYO

Kwa upande wake, meneja mwingine wa Wasafi, Babu Tale alirusha dongo lililotafsiriwa kulenga Fiesta; “Haya mi’ nalala ila kwa wale wasiojua, ni Wasafi pekee ndiyo waliothubutu kumtoa mkoloni kwenye tasnia hii na bado.”

 

FIESTA VS WASAFI FESTIVAL

Kwa takriban miaka kadhaa sasa Tamasha la Fiesta limekuwa likifanyika kila mwaka Bongo ambapo awali lilijulikana kama Summer Jam.

Kwa kipindi chote cha uandaaji wa Fiesta, kulikuwa na lawama nyingi za baadhi ya Wabongo dhidi ya waandaaji wake, Prime Time Promotions chini ya mwamvuli wa Clouds.

Malalamiko mengi yalielekea katika ubaguzi na unyonyaji wa wasanii.

Katika kile kilichoenezwa katika fikra za Wabongo dhidi ya waandaaji chini ya marehemu Ruge Mutahaba, ni kwamba kampuni hii ya uandaaji wa matamasha ambayo pia ilifanya kazi ya kusimamia baadhi ya wasanii ilikuwa ikiwabagua baadhi ya wasanii wengine wasiofanya kazi chini ya mamlaka yao au yale ya wabia wao, Clouds.

 

Pia wakawa wanalalamikiwa zaidi kwa kutoa na kuwaingiza wasanii kwenye mikataba ya kinyonyaji zaidi ambayo iliwanufaisha zaidi wao kuliko wasanii.

Hali hii ilisababisha Wabongo wengi kuwa na shauku ya kupata mwekezaji mwenza kwenye tasnia hiyo ambaye atakayebeba maono yao.

 

Hii ndiyo sababu ya wengi kuipokea kwa mikono miwili Wasafi Festival.

Wengi waliipokea Wasafi kama mkombozi wa wasanii na sababu kuu ni kwa kuwa Wasafi ipo chini ya mwanamuziki ambaye anajua vyema shida na matakwa ya wanamuziki wenzake, lakini sasa inaonekana kuwa makundi yanayokamiana.

 

KUTOKA KWA MHARIRI

Hakuna ubaya wowote kushindana kikazi kwani huko ni kujenga chachu ya kukuza tasnia ya muziki wa Bongo Fleva. Cha msingi ni kujua tu kwamba Fiesta na Wasafi, wote mnajenga nyumba moja hivyo hakuna sababu ya kugombea fito.

Stori: Sifael Paul, Amani

Leave A Reply