The House of Favourite Newspapers

Wasauz wamnyatia Mzamiru Yassin

0
Mzamiru Yassin

TIMU za Bidvest Wits na Mpumalanga Black Aces za Afrika Kusini, zimeanza kumfuatilia kiungo wa Taifa Stars na Simba, Mzamiru Yassin ili ziweze kumsajili baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

Mzamiru ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini akiwa na kikosi cha Taifa Stars, kinachoshiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa), kiwango anachokionyesha kimeonekana kuwavutia mawakala wengi wa nchini humo.

Mitandao pamoja na magazeti mbalimbali nchini humo, imekuwa ikizungumzia kiwango bora kinachoonyeshwa na kiungo huyo ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar.

Akizungumza na Championi Jumatano moja kwa moja kutoka Afrika Kusini, Mzamiru alisema ni kweli amekuwa akisikia tu taarifa hizo, lakini mpaka sasa hakuna mtu wala timu iliyomfuata na kuzungumzia ishu ya kumtaka.

“Hizo taarifa nimekuwa nikizisikia kila siku, lakini mpaka sasa nikwambie tu hakuna timu wala mtu aliyenifuata tukazungumza kuhusiana na wao kutaka kunisajili. “Lakini hata kama wakija, mimi siwezi kufanya chochote zaidi ya kuwaambia waongee na viongozi wangu wa Simba kwani bado nina mkataba nao, hivyo sina mamlaka ya kufanya makubaliano na timu nyingine bila ya kupitia Simba,” alisema Mzamiru.

Stori: Ibrahim Mussa na Said Ally | Championi Jumatano

 

Leave A Reply