The House of Favourite Newspapers

Wastara Asimulia Magufuli Alivyomuokoa

0

MSANII wa sinema za Kibongo, Wastara Juma, amesimulia jinsi aliyekuwa Rais wa Jahmuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk John Pombe Magufuli alivyogusa maisha ya watu wengi ikiwemo kuokoa maisha yake.

 

Akizungumza na RISASI MCHANGANYIKO jana, Wastara alisema, Hayati Rais Magufuli ataendelea kuishi kwenye mioyo ya watu wengi kwani aliamua kujitoa sadaka kwa wengine na kwa upande wake, aliokoa maisha pale alipokuwa akisumbuliwa na tatizo la mgongo na mguu.

 

“Yani kwa kweli nashindwa hata namna ya kuelezea maana Rais Magufuli (hayati) alijitoa sana. Wewe angalia wakati ule mimi naumwa mguu na mgongo, aliona kwenye mtandao nilipoomba msaada na hapohapo alichukua hatua za haraka.

 

“Aliwatuma wasaidizi wake mpaka nyumbani kwangu Tabata na kuniletea shilingi milioni 15 cash ambazo walitoa yeye pamoja na mke wake mama Janeth.

“Kwangu mimi wakati ule sikuwa na njia yoyote ya kupata hizo pesa maana zilikuwa zinahitajika na sikuwa nazo. Kwa kweli Mungu amlaze mahala pema peponi yule baba kwani alikuwa na moyo wa kipekee,” alisema Wastara.

 

Akiendelea kuzungumza na RISASI MCHANGANYIKO, msanii huyo alisema kuwa kutokana na maumivu ambayo anayo, ameamua kuingia studio na kumtungia wimbo pamoja na kurekodi video yake ambapo anaona angalau itampa ahueni ndani ya moyo wake.

 

“Nimeingia studio na tayari nimesharekodi wimbo audio na video, wimbo unaitwa Dunia Imesimama na bado nilichofanya naona hakitoshi kumuenzi, naumia mimi sana na sidhani kama kuna mtu ananielewa,” alisema Wastara.

 

Sanjari na Hayati Rais Magufuli, wasaidizi wa aliyekuwa kiongozi huyo wa nchi, walichangia shilingi milioni moja.Wastara alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mguu kusagika baada ya kuwekewa mguu wa bandia kufuatia mguu wake mmoja kukatwa baada ya kupata ajali miaka mingi iliyopita.

 

Baada ya kuwekewa mguu huo wa bandia nchini India, alikuwa akitakiwa kurudi kliniki baada ya kipindi fulani lakini ilifika wakati alishindwa kurudi kwa sababu ya kutokuwa na fedha.

 

Kitendo cha yeye kukosa fedha ndicho kilichosababisha apate tatizo lingine la maumivu ya mgongo na kulazimika kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuomba Watanzania wamsaidie ili aweze kupata kiasi kisichopungua shilingi milioni 37.

 

Baada ya wadau wengine kujitolea na kufikia kiasi fulani ndipo Hayati Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth walipoguswa na kukamilisha fedha hizo kisha Wastara akaenda India haraka kupatiwa matibabu na baadaye kurejea nchini Marchi 01, 2018.

 

Wastara ni mjane baada ya kufiwa na mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’ miaka mingi iliyopita. Mumewe huyo naye alikuwa msanii na muandaaji wa filamu Bongo.

Leave A Reply