Watanzania Washauriwa Kwenda Kufanya Utalii wa Ndani Katika Hifadhi ya Taifa Mikumi
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imevunja rekodi ya kupokea watalii ambapo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2024 imepokea watalii 76,000 huku ikitarajia kupokea watalii 123,000 hadi kufika Julai, 2024.
Hayo yamesemwa na Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Utalii wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei ambapo amesema Filamu ya The Royal Tour imekua chachu kubwa katika kuhamasisha utalii.
Hifadhi ya Mikumi ipo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambapo kutokana na kuwepo kwa miundombinu bora ya usafiri ya reli ya kati, uwanja wa ndege ndani ya hifadhi hiyo na Barabara Kuu ya TANZAM (Morogoro -Iringa) kumesaidia kuwepo kwa ongezeko la watalii.
Amesema kwa siku, hifadhi hiyo inao uwezo wa kupokea watalii 200 hadi 250, tofauti na miaka ya nyumba kabla ya ujio wa Filamu ya The Royal Tour ambapo kwa sasa hamasa ni kubwa na watalii wazawa wanazidi kuongezeka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishina Agustine Masesa amesema kitendo cha watalii wazawa kufika katika Hifadhi ya Mikumi ni kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta ya utalii.
“ Mheshimiwa Rais ametuonesha njia, sasa ni wakati wetu sisi Watanzania kutembelea hifadhi zetu, rais anatoka ikulu kwenda mbugani, wewe ni nani usije?”
Amesema katika hifadhi hiyo kuna viwanja vya michezo mbalimbali ambapo wasanii wanashauriwa kurekodi nyimbo zao na filamu badala ya kwenda kurekodi nje ya nchi.
Msisitizo kwa jamii ni kuendelea kujitokeza kwa wingi kuunga mkono jitihada za Rais Samia kutangaza utalii wa ndani katika nchi mbalimbali.