The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-21

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
Nilifika mbali nikaligeuza gari na kurudi. Nilipita tena ile nyumba nikaenda kusimama umbali wa mita mia tatu hivi. Nililiegesha gari pembeni mwa barabara. Nikavua nguo zangu mlemle ndani ya gari kisha nikatoka nikiwa na mkoba wangu.

Nililizunguka lile gari langu mara saba ili mtu yeyote akipita pale asilione. Nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea katika nyumba ya waziri mkuu. Usiku huo kulikuwa kimya kiasi kwamba niliweza kutembea nikiwa mtupu bila wasiwasi wowote.
SASA ENDELEA…

H
ata hivyo kulikuwa na dawa zilizokuwa zikinikinga nisionekane waziwazi. Kama kungekuwa na mtu anaangalia barabarani wakati huo na kuniona, angeona paka au mbwa na asingeniona mimi.

Uchawi huo nilifundishwa na babu yangu. Kulikuwa na dawa ambayo ninajipaka mwili mzima ambayo husababisha kiini macho kwa mtu yeyote ambaye ananitazama.
Babu alinifundisha uchawi huo ili ninapokwenda katika safari zangu za uchawi wakati wa usiku nisiweze kuonekana.

Babu pia alinifundisha kuzitahadhari nyumba zilizowekwa mazindiko. Aliniambia kuwa ninaweza kunasa au kuanguka na kushindwa kuinuka.

Lakini sikutarajia kuwa nyumba anayokaa waziri mkuu ambayo ilikuwa nyumba ya serikali ingewekewa zindiko hata kama waziri mkuu mwenyewe angekuwa mswahili.

Nilipofika katika nyumba hiyo, sikutokea kwa mbele ambako kulikuwa na geti, nilitokea kwa nyuma. Hatua tatu kabla ya kuufikia ukuta uliozunguka nyumba hiyo nilirusha vipimo vyangu ambavyo vilionesha kuwa nyumba hiyo ilikuwa salama kwa maana kwamba haikuwa na zindiko lolote ambalo lingenizuia kufanya nilichotaka kufanya.

Nikasogea katika ukuta huo na kujigandamiza huku nikinuia kupenya ukuta huo. Wakati huo nilikuwa nimefumba macho yangu na kuzielekeza hisia zangu kwamba naupenya huo ukuta kwa nguvu za uchawi.

Kufumba na kufumbua nikajikuta niko upande wa pili wa ukuta huo, yaani tayari nilikuwa nimeshapenya ndani na kutokea kwenye ua wa nyumba ya waziri mkuu.
Nilitulia kwa sekunde kadhaa nikiangalia kila upande. Nyumba ilikuwa kimya na sikuona mtu yeyote.

Hali hiyo ilinionesha kwamba wenyewe walikuwa wamelala na hiyo ilinipa furaha kwamba ningeweza kufanya mambo yangu vizuri.

Nikazunguka kwenye mlango wa mbele kwa hatua za haraka. Nikiwa kwenye mlango huo, geti la kuingilia na kutokea nje lilikuwa mbele yangu. Geti hilo lilikuwa limefungwa na kulikuwa na polisi wawili mbele ya geti upande wa nje waliokuwa wamekaa kwenye viti wakivuta sigara.

Nikajigandamiza kwenye mlango wa nyumba hiyo kama nilivyofanya kwenye ukuta. Nilikuwa nimefumba macho yangu na kunuia kuwa ninapenya kwenye mlango huo.
Hapo hapo nikajikuta nimeshaibukia ndani. Nilitokea kwenye sebule pana la waziri mkuu. Sikuwahi kuingia ndani ya nyumba yake, ile ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza.

Nilishangaa kukuta sebule ya nyumbani kwangu ilikuwa nzuri kuliko sebule hiyo. Ilikuwa na fanicha zisizo na thamani na siyo zile ambazo mtu yeyote angetegemea kuzikuta nyumbani kwa waziri mkuu.

Nilijua ile ilikuwa janja yake ili aonekane kuwa hatumii vibaya pesa za serikali. Kuweka fanicha duni ilikuwa ni kuwazuga tu wageni waliokuwa wanafika nyumbani kwake.
Wakati ninaizungushia macho ile sebule nilishtuka na kushangaa kumkuta waziri mkuu ameketi kwenye moja ya makochi yake ya bei rahisi akiwa na laptop yake mapajani.

Kitu kingine kilichonishangaza ni kuona ameshika sigara iliyokuwa inafuka moshi. Siku ile ndiyo nilijua kuwa waziri mkuu alikuwa anavuta sigara. Mawaziri wote tulikuwa tunajua kuwa waziri mkuu wetu hakuwa mvutaji. Kumbe alikuwa anavuta kisirisiri kwa kuhofia kujiharibia hadhi yake.

“Kumbe huyu bwana halali usiku na anavuta!” nikajiambia kimoyomoyo huku nikimkodolea macho bila yeye kuniona.

Kwa vile nilimkuta mwenyewe yuko macho, nisingeweza kumuwangia mbele yake, nikarudi nje ya mlango. Hapo nikaanza kucheza ngoma yangu ya kichawi ya kumuwangia. Punde tu waziri mkuu akaanza kusinzia.

Nilipogundua kuwa nilikuwa nimeshamtia usingizi ndipo nilipoingia tena sebuleni. Nilimfuata waziri mkuu aliyekuwa akisinzia bila kuizima laptop yake. Nikamzunguka mara saba huku nikimputia kwa mwengo wangu wa kichawi niliokuwa nimeushika kwa mkono wangu wa kushoto.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Leave A Reply