The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-38

1

Asubuhi alinikumbushia yaliyotokea usiku uliopita.
Akaniuliza tena wale watu walikuwa akina nani. Majibu yangu yalikuwa yale yale niliyompa jana usiku.

Muda wetu wa kwenda kazini ulipowadia tukatoka. Niliuona uso wa mke wangu haukuwa wa kawaida. Ulikuwa na kitu kama tuhuma dhidi yangu lakini hakutaka kuniambia yaliyokuwa moyoni mwake.
SASA ENDELEA…
Kwa mara ya kwanza tangu nilipoanza kujifundisha uchawi nilianza kukosa raha. Nilihisi kwamba wale watu wangerudi tena na pia sikuwa na kinga ya kuzuia mtoto wangu asichukuliwe kiuchawi na wachawi hao.

Mpaka narudi kazini jioni sikuwa nimepata ufumbuzi wa suala hilo. Nilikuwa mnyonge sana na mke wangu pia hakuwa na amani.
Wakati tunakwenda kulala usiku aliniuliza:
“Wale watu hawatakuja leo?”

“Hawawezi kuja tena, usiwe na wasiwasi.”
Usiku wa jana yake nilisali mimi, mke wangu akawa ananitazama. Usiku ule ulikuwa zamu ya mke wangu. Alisali sana.

Badala ya kumlaza mtoto wetu kwenye kitanda chake alimlaza katika kitanda tunacholala sisi. Nikaona alikuwa amemvalisha msalaba wa fedha shingoni.
Nikahisi alikuwa na wasiwasi na wale wachawi waliokuwa wanataka kumchukua Mkanga.

Wakati tulipokuwa tumelala, niliota wale wachawi wameingia ukumbini mwa nyumba yetu wakicheza ngoma zao za kichawi. Kelele walizokuwa wakipiga ndizo zilizoniamsha mimi na mke wangu.

Nilipoamka na kufumbua macho nikasikia zile kelele zinasikika ukumbuni kweli kama nilivyoota.

“Hawa watu wapumbavu kweli, wameshaingia ndani!” nikajisemea peke yangu.
Ingawa nilisema kwa sauti ya chini lakini nilisikia mchawi mmojawapo akinijibu kutoka ukumbini.

“Sisi si wapumbavu, tumefuata mtoto wetu. Usipotupa tutaingia hadi humo chumbani tumchukue wenyewe.”

Mke wangu aliyasikia yale maneno akawa analia huku amemkumbatia Mkanga.
Mkanga mwenyewe alikuwa amelegea kama mnyoo na jasho jembemba lilikuwa likimtoka. Nikajua sasa Mkanga anakwenda!

Kutokana na kuhamaki nilichukua simu yangu nikampigia yule mlinzi kwa haraka.
Nilijua kama nitachelewa kuchukua hatua, wachawi hao wataniingilia chumbani. Kama wameweza kupenya ukumbini wasingeshindwa kujipenyeza chumbani.
Mlinzi akapokea simu.

“Wale watu wamekuja tena. Hivi sasa wameingia ukumbini,” nikamwambia yule mlinzi.
“Wameingilia kwa wapi” Mlinzi akaniuliza.
“Sijui wameingilia kwa wapi lakini wako ukumbini. Sasa njoo hapa kwenye dirisha nikupe funguo ufungue mlango wa mbele uingie ndani uwapige risasi.”

Mlinzi akaja kwenye dirisha kwa haraka. Nilifungua dirisha nikampa funguo kwa dirishani. Mlinzi akaenda kufungua mlango wa mbele na kuingia.
Zile kelele zilizokuwa zinasikika zikatoweka ghafla. Nikaenda kwenye mlango wa chumbani na kuufungua kisha nikachungulia ukumbini. Nilimuona Mlinzi amewasha taa akitafutatafuta.

“Nimeingia lakini sijaona mtu mheshimiwa,” akaniambia.
Mke wangu naye akatoka.
“Watu walikuwepo wanataka kumchukua mwanangu,” akasema kwa hofu huku akiendelea kulia.

“Sasa hao watakuwa ni akina nani na wameingilia kwa wapi bila mimi kuwaona?” Mlinzi akauliza kwa mshangao.
“Watakuwa ni wachawi. Wameingia humu ndani kiuchawi, huwezi kuwaona. Tangu juzi wanakuja.”
“Kama ni wachawi tutawazuiaje?”
Mke wangu hakujibu swali hilo, akarudi chumbani.
“Hawa watu watatusumbua,” nikajidai kusema huku nikiwa nimefadhaika.
“Kama ni wachawi watatusumbua kweli.”

“Wewe hujui dawa za kuwazuia?” nikamuuliza yule mlinzi.
Mlinzi akatikisa kichwa.
“Hapana. Mimi sijui kitu.”

“Kwa kweli watanisumbua. Sijui nitafanya nini?” nikasema kisha nikamwambia Mlinzi anipe ule ufunguo niliompa.
Aliponipa nilimwambia: “Basi wewe nenda.”

Mlinzi akatoka. Mimi niliogopa kurudi chumbani nikaenda kukaa sebuleni. Niliogopa kurudi chumbani kwa sababu nilijua mke wangu alikuwa akinisubiri anishambulie kwa maneno na ugomvi wake ungekuwa mkubwa.
Pale sebuleni nilifungua TV, nikawa ninatazama taarifa mbalimbali za nje. Usingizi ulikuwa umeniruka.

1 Comment
  1. Aisha Chumo says

    Mpaka wamchukue dah

Leave A Reply