Yanga Yafungukia Pengo la Litombo na Aucho

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, ameweka wazi kuwa kukosekana kwa baadhi ya nyota wa kikosi hicho ambao wapo kwenye majukumu ya timu za taifa wakiwemo, Khalid Aucho na Yanick Bangala Litombo hakujaathiri maandalizi ya kikosi hicho kuelekea mchezo wao dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

 

Baadhi ya nyota wa Yanga ambao wamekwenda kujiunga na timu zao za taifa ni Dickson Job, Litombo, Feisal Salum, Aucho, Ramadhani Kabwili na Bakari Mwamnyeto.

 

Katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga watacheza dhidi ya Rivers United Septemba 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa kabla ya kurudiana nao Septemba 19, mwaka huu huko Nigeria.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwakalebela alisema: “Kikosi chetu kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Septemba 12, mwaka huu.

 

“Licha ya kwamba kuna baadhi ya wachezaji ambao wamekosekana kutokana na majukumu ya timu za taifa kwa ajili ya michezo ya kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia, lakini niwatoe hofu mashabiki wa Yanga kuwa, tuna kikosi bora na kutokuwepo kwa nyota hawa, hakujatuathiri kwa namna yoyote.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam.


Toa comment