The House of Favourite Newspapers

Zuchu Awafunika Wabunge

0

UMAARUFU na mafanikio ya msanii kinara wa kike kwa sasa kwenye Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’, vinatajwa kuwafunika hadi wabunge wapya, wanawake walioingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka huu.

ZUCHU MWENYEWE ANASHANGAA

Hata Zuchu mwenyewe anashangazwa na ripoti za mitandao mingi ya habari za mastaa Afrika kumtaja kama msanii maarufu zaidi kwa sasa Afrika Mashariki.

Imeelezwa kwamba, katika kipindi cha miezi sita tu alichodumu kwenye muziki huo tangu aliposainiwa ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameweka rekodi za kila aina ndani na nje ya Tanzania.

Kuna kituo kimoja cha runinga nchini Hispania kimefikia hatua ya kumpachika jina la Beyonce wa Tanzania akifananishwa na mwanamuziki Beyonce Knowles wa Marekani.

Mitandao hiyo imemtaja Zuchu kama mmoja wa wasanii waliochangia kukuza muziki wa Bongo Fleva kwa kutoa nyimbo za mapenzi zilizochanganywa na midundo ya kisasa inayotokana na muziki wa jadi wa Taarab kutoka Pwani ya Afrika Mashariki.

UMAARUFU

Kwa mujibu wa mitandao hiyo, Zuchu ni msanii mwenye bidii na shoo zake zimekuwa zikivutia mashabiki wengi ambao baadhi ya wabunge wapya waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu na wale wa Viti Maalum, hawana uwezo wa kukusanya umati mkubwa kama anavyofanya Zuchu.

Zuchu anatajwa kuwa amejizolea umaarufu mkubwa kutoka kwa watu wengi wenye uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii ambao inakisiwa kufikia asilimia 25 ya idadi ya Watanzania wote ambao ni milioni 60 (kwa mujibu wa takwimu za Februari, mwaka huu).

Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa, kuna mashabiki wengi wanaopenda muziki wa Bongo Fleva walio tayari kusikiliza muziki wake wa mapenzi.

 

WAFUASI

Hadi juzi, Zuchu alikuwa na zaidi ya wafuasi milioni 1.4 kwenye Mtandao wa Instagram na zaidi ya laki 5 kwenye YouTube ambao asilimia kubwa ya baadhi ya wabunge hao, hawana.

Zuchu anaendelea kuachia muziki kila kukicha huku akifanya matamasha makubwa sehemu mbalimbali za Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

 

WATAZAMAJI MIL. 64

Mpaka sasa, Zuchu ametazamwa mara zaidi ya milioni 64.8 katika chaneli yake ya YouTube, huku akiwa mwanamuziki pekee wa kike Afrika Mashariki anayeongoza kwa kutazamwa kwenye YouTube kwa miezi sita mfululizo ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo, Zuchu anaweka rekodi hizo kwa sababu ya bidii yake kubwa ambayo anatumia kukuza sanaa yake ya muziki.

Zuchu amekuwa akiweka rekodi za kipekee, hususan kwa mwanamuziki mwenye muda mfupi zaidi kwenye kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva.

MAFANIKIO

Kwa mujibu wa wataalam wa IT, Zuchu ameongoza kwa miezi sita mfululizo kwa kusikilizwa ambapo amekuwa akiingiza kati ya Dola za Kimarekani 1,900 (zaidi ya shilingi Mil. 4.3 za Kitanzania) hadi Dola za Kimarekani 29,000 (Zaidi ya shilingi Mil. 66 za Kitanzania) kwa mwezi, pesa ambazo hakuna mbunge anayeingiza kiasi hicho.

 

Miongoni mwa nyimbo za Zuchu zilizotazamwa zaidi na kumuingizia mkwanja mrefu ni Raha, Wana, Nisamehe, Cheche, Litawachoma, Hakuna Kulala, Mauzauza na nyingine kibao.

 

ZUCHU VS WABUNGE

Imeelezwa kwamba, Zuchu ana uwezo wa kukusanya wafuasi wengi zaidi ukilinganisha na baadhi ya wabunge wapya ambao bado hawajapata hata majina makubwa bungeni.

“Chukua mfano Zuchu aseme ana jambo lake pale Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar) uone watajitokeza watu wangapi, halafu baada ya wiki moja ajitokeze mbunge yeyote katika hawa wapya, naye aseme ana jambo lake uone ni watu wangapi watajitokeza.

“Kwa Zuchu kutakuwa na nyomi kubwa mno, lakini kwa huyo mbunge mpya ataambulia watu mia au mia mbili,” anasema Happyness Masunga, mwandishi na mchambuzi wa habari za burudani nchini Tanzania.

Kwa upande wa mapato, Zuchu anatajwa kuwa na uwezo wa kuingiza hadi zaidi ya shilingi milioni 60 kwenye Mtandao wa YouTube pekee, bila mitandao mingine na shoo ambapo dau lake kwa ajili ya shoo moja siyo chini ya shilingi milioni 20 za Kitanzania.

“Lakini kwa upande wa wabunge hao, kwa mujibu wa chanzo chetu cha uhakika ambacho ni mbunge, mshahara wa mbunge kwa mwezi ni shilingi milioni 3.8 za Kitanzania.

Pia wabunge wana posho ya Ubunge ambayo ni shilingi milioni 8 kwa mwezi, posho ya kujikimu ni shilingi laki 120,000 kwa siku na kukaa kikao cha bunge, posho ni shilingi laki 200,000 kwa siku.

Imefahamika kwamba, wakati Zuchu akiingiza zaidi ya shilingi milioni 60 kwenye YouTube pekee, kipato cha juu cha mbunge ni shilingi milioni 12 kwa mwezi.

Hata hivyo, mbunge yeye ana kiinua mgongo baada ya miaka mitano ambacho ni shilingi milioni 240 huku akiambulia pesa ya mfuko wa jimbo ambazo ni shilingi milioni 46 za Kitanzania.

 STORI: KHADIJA BAKARI

Leave A Reply