The House of Favourite Newspapers

Shoga, Una Nguvu Kubwa, Itumie

Na MWANDISHI WETU| RISASI MCHANGANYIKO| SHANGINGI| LOVE SMS

HALOHALOO watoto wa kike popote mlipo, hamjamboo? Shangingi wenu mstaafu leo nimechoka hatari, maana jana sikulala mwenzenu, tumelicheza segere pale kwa Bii Mwantumu hadi basi, si alikuwa anamtoa mwari, basi nimechoka acha tu! Sasa nimekuja nimejitupa hapa barazani, mara kama kawaida, wamejaa, kila mtu na umbeya wake.

Nilichowapendea leo, kwa pamoja wameniomba niwape neno lolote ambalo litawasaidia katika harakati zao za kimapenzi, maana wengi bado vijana, wa motomoto, wenyewe wanasemaga bado wananuka maziwa ya mama. Kuna neno moja la msingi sana naweza kuwapa, ni kutambua nguvu kubwa waliyonayo watoto wa kike, kwenye kila kitu.

Mnajua wazi kabisa kuwa hatuna nguvu za mwili za kuweza kupambana au kufanya kazi kama wanazofanya vijana wa kiume, lakini tunayo nguvu inayozidi tani hata elfu moja ya mawe. Nguvu ya mwanamke iko kwenye uanamke wake, lakini uzuri wa umbo, elimu, sura, sauti na hata mwendo ni nyongeza nyingine inayokuongezea nguvu hizo. Kwa ajili hiyo, ni makosa makubwa kuona mtoto wa kike anapata tabu katika maisha yake, anakosa anachohitaji au anashindwa kufikia malengo yake.

Nguvu za mwanamke hazipo katika kupigana, la hasha, bali zipo katika kushawishi, kwa maneno na hata vitendo, achilia mbali hisia.

Kuna jambo moja linalosababisha watoto wa kike wanakosa uwezo wa kutumia nguvu walizonazo kwa ajili ya maisha yao, kukosa nidhamu.

Wadada wengi na akina mama wanakosa nidhamu katika maisha yao, kitu kinachosababisha wanapoteza nguvu zao na hivyo kugeuka kuwa dhalili.

Nidhamu ninayoizungumzia ni ile ya maisha yao binafsi. Mtoto wa kike unapaswa kujiheshimu kwanza wewe mwenyewe, unapaswa kuuogopa mwili wako usigusweguswe ovyo na wanaume, uupende. Hata kama huna uwezo wa kusuka nywele saluni, unaweza kubaki na ubora wako. Mwanamke anayejiheshimu, anawatisha wanaume.

Namna mwanamke anavyojiweka, ndivyo mwanaume anavyomchukulia. Ukiwa mtu rahisirahisi, nao wanakuja kirahisirahisi, ukiwa makini, unawapa wakati mgumu sana kukusogelea, maana hawana uhakika kama watakupata au la.

Na nikuambie kitu, hakuna kitu kinawauma wanaume kama kukataliwa, ni bora akae kimya asikutongoze  kuliko atupe ndoana zake halafu akukose.

Kwa hiyo ili uweze kuonyesha nguvu yako, ni lazima ujiheshimu. Ukijiheshimu, mwanaume atakayekuja, atakuwa anajiamini.

Na katika mazungumzo ukimuelewa, basi unaweza mwambia unachotaka, kwa mfano siwezi kujiingiza katika mapenzi sasa hivi, natafuta kazi kwanza ili niweze kumsaidia mama yangu.

Mwanaume anaweza kujiingiza mwenyewe kuwa atakutafutia kazi na mama yako atamsaidia. Vivyo hivyo pia kama unataka kujiendeleza kielimu na vitu vingine. Lakini kama wewe kazi yako ni mwepesi, mwenye kutaka hela tu kila siku, watakuchukulia hivyo hivyo, wanakupa hela, wanapata wanachotaka halafu wanakuacha!

 

Comments are closed.