The House of Favourite Newspapers

SHOGA; Unajua Mzee Anapenda Nini Kwenye Chakula?

0

Na SOPHIA MA`MDOGO| GAZETI LA UWAZI| MAKALA

NI Jumanne nyingine shoga nimekutana nawe kwenye kona yetu hii ya mahaba, kona ya mashamsham, kona pendwa ya watu wote wapenda elimu ya mapenzi, upo shoga?

Kiafya shoga kama ulivyoniacha jana, nimejaa tele sijui mwenzangu wewe, u mzima? Kama ni mgonjwa basi tuombeane kwa Muumba najua utapata wepesi au siyo shoga yangu, maana mi na wewe tena, kama kuku na vifaranga vyake, eeehee eheee hiyaaaa!!

Basi shoga kila nikitaka kukaa kimya mdomo unanicheza kama siyo kunitekenya, kama ujuavyo mwenzangu kukaa kimya siwezi moja kwa moja lazima nitie neno ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, upo?

Leo shoga langu la ukwee wangu nataka niwape somo la bureee kuhusu kulinda nyumba zetu hasa kwenye hiki chakula cha usiku. Tumekuwa tukilalamika tu kuwa wazee wetu hawaoneshi kufurahia mapenzi tukiwa tunakula chakula chetu kile cha usiku.

Niliwahi kuwaelezea kuhusu kupewa uhuru, sasa umeupata ufanyie kazi. Inawezekana uliyenaye ni mgeni katika kuandaa chakula cha usiku, nawe kama siyo mbunifu wa kujua uliyenaye ni ‘kijiko au sahani’ basi chakula chenu kinakuwa bora ushibe tu.

Waweza usione hasara zake mapema, lakini hasara zake huwa kubwa ndicho chanzo cha nyumba nyingi kuyumba au kusambaratika kabisa. Unajua sababu gani? Nakuuliza acha kunitumbulia mijicho kama fundi saa aliyepoteza lensi. Siku zote sisi wenyewe ndiyo tumekuwa wanga wa uhusiano na ndoa zetu bila kujua.

Hebu kaa chini nikupashe shoga ili usichelewe, pamoja na kumpikia chakula kitamu basi ongeza cha ziada uamshe furaha na kumfanya mwenzako achanganyikiwe na kuona mambo mapya ya msosi. Si wote mmepitia unyagoni na kupata mafunzo ya kupika chakula cha usiku, jamani mafunzo ya chakula ukiyajua nina imani ndoa yako kila siku itakuwa mpya.

Katika maisha ya ndoa hasa ya kupika chakula lazima mwakwetu ujue wazee wanapenda nini. Na hii utaijua pale mzee wako wa kwanza utakaye kula naye raha umuulize kijanja vitu gani wazee wanapenda siyo kukurupuka kama unatoka kujisaidia kichakani, heee heee heiiiyaaa, upo? Siku zote mjenzi mzuri hujifunza tabia za udongo ili akijenga nyumba isianguke haraka au kuweka nyufa.

Hata katika kutengeneza chakula ili kula na mwenzako hebu jenga tabia ya kudadisi anapenda uweke nini? ”Mzee nikikuwekea nini kwenye chakula unapenda?” lazima atakujibu vilevile nawe una haki ya kumueleza mpenzi wako kuwa: “Mzee wangu usisumbuke sana kula chakula changu chote, kuna sehemu ukila lazima utasikia ladha ya pilipili na lazima nikohoe tu.”

Shoga siyo mtu anakuwekea kitu kwenye chakula wala huwashwi wala kujisikia chochote, wewe nawe? Kwa vile hajui basi utajikuta mpaka mnaanza kula chakula wee upoupo tu shoga yangu! Haipendezi shoga hebu basi tuambiane ukweli ili kuzifanya nyumba zetu wakati wote kuwa na furaha.

Kuna maeneo mengi ya mambo ya mezani unatakiwa kuyajua mkiwa kwenye uwanja wa fundi seremala. Unapoona hutendewi haki mweleze mwenzako ili ajue siyo kukaa kimya unaumia moyoni kumbe ulitakiwa kusema. Wengi hulalamika hawajawahi kuhisi ladha ya chakula cha usiku tangu waolewe hata wengine kudiriki kusema huwa hawashibi hadi chakula kinaisha kabisa, mmh! Shogaaaa!

Narudia kauli yangu siyo wote wanaojua kula chakula, hebu muulize mtu aliyekuzidi amewezaje kufurahia chakula cha usiku siku zote. Akiisha kueleza basi lifanyie kazi ndani, haki ya nani utashangaa kumuona mtu mzima akilia kama mtoto mdogo si kwa kupigwa bali njaa ya kula chakula.

Utashangaa unapata ambavyo hukuwaza kupewa, la muhimu ni kukubali kujifunza na kuyafanyia kazi hakika kila siku ndoa yako itakuwa mpya. Shoga nisiwe muongeaji sana, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine tamu zaidi ya hapa!

Leave A Reply