The House of Favourite Newspapers

Diva, Ukubwa Haupigi Hodi

0
Diva (Kushoto) akiwa na rafiki yake.

MOJA kati ya vitu ambavyo binadamu ameshindwa kuvizuia, ni kukua kwake, kiakili na kimwili. Ukiondoa matatizo ya kiafya yanayoweza kufanya vinginevyo katika mwili wa binadamu, ilivyo ni kwamba kadiri anavyoongezeka umri, akili yake hupanuka zaidi na kuongeza maarifa, tofauti na zamani.

Diva

Tofauti na miongo michache iliyopita, teknolojia hivi sasa imekua kwa kiwango kikubwa, kiasi kwamba dunia imekua kijiji. Kupitia simu ya mkononi, mtu anaweza kuona kitu kinachotokea sehemu yoyote katika dunia hii.

Teknolojia hii, imekuwa nzuri zaidi kwa wafanyabiashara, kwani wanaweza kuitangaza kutoka China, ikapata mteja Tanzania. Au wanafunzi, ambao wanaweza kujifunza vitu vingi ambavyo pengine hata walimu wao hawana vichwani mwao.

Ninamtazama Loveness Diva Malinzi, kama mmoja wa watu wanaonufaika sana na kukua kwa teknolojia, kwani licha ya kuwa ni mtangazaji mahiri, anayesikika karibu dunia nzima, bado anajitangaza kupitia mitandao ya kijamii, kwenye akaunti zake! Tatizo langu na Diva ni vile anavyoitumia akaunti yake katika Mtandao wa Instagram.

Bahati mbaya sijawahi kusikia biashara nyingine anayoifanya zaidi ya kazi yake ya utangazaji, ingawa katika moja ya interviews zake, niliona sehemu akisema hapo baadaye anatamani kuwa na Boutique kubwa! Nisingekuwa na tatizo kama angekuwa ni model, mithili ya akina Miriam Odemba, Flaviana Matata au Millen Magese maana hawa wanapata hela kwa sababu ya shepu zao, kwani wanayavutia makampuni ya mitindo yanayotaka kutangaza bidhaa zao mbalimbali.

Unapoingia katika ukurasa wake, unakutana na picha ambazo kibongobongo, hazifai. Zinaonyesha sehemu kubwa ya mwili wake, kitu ambacho kwa heshima ya jina la familia yao (ni mwanafamilia ya Malinzi, akiwemo Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi) angejiheshimu.

Kuna watu pembeni wanasema anatangaza biashara, ukiwauliza biashara gani hawasemi. Maana kuna picha zingine zinaonyesha kitovu, zingine mapaja yake, zingine sehemu ya mgongo wake na zingine za kila namna, ili mradi,
kwa mtu mwenye heshima zake, zinamchefua! Kuna wasichana wengi mtaani wanafanya biashara ya kujiuza kupitia mitandao.

Wao wame-advance zaidi kuliko Diva, maana wengine wanatupia picha wakiwa watupu kabisa. Lakini hawa unaweza kuwasamehe kwa sababu wanatoka familia masikini, hawana kazi na wala hakuna awajuaye. Sasa unapokutana na Diva, akitupia picha zinazofanana na hizo, unapata shaka kidogo na kichwa chake, huenda anadhani yeye bado ni mdogo, hivyo ni haki yake.

Hapana, hata kama ana umri wa ujana, hadhi yake inamfanya kuwa tofauti na historia ya familia yake pia inamtoa katika kundi lile la akina wale, ambao ili mkono uende kinywani, ni lazima mwanaume afungue waleti yake.

Unachopaswa kujua ni kuwa wanaume wa kweli wanawadharau wasichana wanaoachia miili yao ovyo mitandaoni. Na mara nyingi, wanawahitaji kwa ajili ya starehe tu za muda mfupi.

Kama ni hivyo, ina maana Diva hutaki kuolewa? Huna haja na watoto?

Leave A Reply