The House of Favourite Newspapers

Thamani ya Samatha Yazipiku Simba, Yanga

Mbwana Samatta

WASWAHILI wanasema kipato huongeza majivuno na ukiona mtu kipato kimekuwa kikubwa na bado anaendelea kuwa muungwana, basi mheshimu sana.

Mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta, anaweza kuwa mfano kwa kuwa thamani yake kama atatakiwa kuuzwa kutoka katika timu yake ya sasa, ni euro milioni 2.2 (zaidi ya Sh bilioni 5.1). Tayari Samatta si yule wa zamani, si yule wa Simba wala TP Mazembe kwa kuwa kama atauzwa kwa kiasi hicho, fedha hiyo ni bajeti ya kuziendesha Yanga, Simba na Azam FC kwa msimu mzima wa Ligi Kuu Bara au mwaka mzima wa michuano yote.

Bajeti ya Yanga kwa msimu mzima ukiweka michuano ya nyumbani na kimataifa ni Sh bilioni 2, hali kadhalika Azam FC pia. Lakini Simba, bajeti yao imekuwa takribani Sh bilioni 1.2. Kama unakumbuka, Mfanyabiashara Mohammed
Dewji ‘Mo’, wakati ametangaza kuinunua Simba alisema anataka kuongeza bajeti ya Simba ifikie Sh bilioni 3 kwa mwaka na kuzipiku Yanga na Azam FC akiamini hiyo itaisaidia kuwa bora zaidi.

TP Mazembe, bajeti yao huanzia Sh bilioni 4.5 hadi Sh bilioni 6.7 kwa msimu. Jambo unaloweza kusema thamani ya Samatta ndiyo inalingana huko. Samatta ameendelea kuongeza juhudi akiwa ni mtu anayejitambua kwamba kila anavyofanya vizuri zaidi basi thamani yake inapanda juu zaidi.

Mtandao mmoja maarufu wa kuchanganua thamani za wachezaji, umeeleza Samatta amekuwa akipanda kwa kasi kubwa kithamani kutokana na mwenendo wake kuwa mzuri. Kwa mujibu wa mtandao huo, Mei 13, 2012 wakati akiwa TP Mazembe, thamani yake ilikuwa euro 200,000 (zaidi ya Sh mil 469).

Ilipofikia Septemba 3, 2012 bado akiwa timu hiyo ya DR Congo, thamani yake ilipanda hadi kufikia euro 500,000 (zaidi ya Sh bilioni moja).

Thamani ya euro 500,000, iliendelea kubaki hadi Juni 23, 2015, lakini Februari 7, 2016 wakati amejiunga na Genk na kuanza kuonyesha angekua na kufanya vizuri baadaye, thamani yake ilipaa haraka na kufikia euro 800,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.8).

Samatta kwa kuwa alielewa anachokifanya, aliendelea kujituma na kupambana zaidi na ilipofikia Juni 15, 2016, thamani yake ilifikia euro milioni 1.5 (zaidi ya Sh bilioni 3.5). Kwa kuwa aliona amezidi kupanda thamani na kwa kuwa alianza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, alizidisha ufanisi na Januari 21, 2017, makadirio yake ya thamani yakafikia hiyo Sh bilioni 5.1.

Pamoja na thamani hiyo kubwa zaidi ya mwanamichezo mwingine yeyote wa Tanzania kwa sasa, Samatta amejiwekeza na tayari ameonyesha kuijali jamii anayotokea kama mtu anayekumbuka alikotoka.

Pamoja na kwamba amekuwa akificha sana, taarifa za uhakika kutoka kwao zimeeleza amejenga msikiti kwao Mbagala. Chanzo cha ndani ya familia kimethibitisha hilo.

“Ni kweli, nafikiri kila kitu kimeisha na limebaki suala la kukabidhi. Lakini vizuri tuliache siku ikifika, atalizungumzia mwenyewe.” Katika maisha ya kawaida, Samatta ni mtu mtaratibu na asiyependa makuu lakini amejiwekeza akimiliki magari ya kifahari kuonyesha anataka kuridhisha nafsi yake kutokana
na juhudi anazofanya.

Anamiliki magari matano yakiwemo ya kifahari kama Range Rover, Chrysler Crossfire na Toyota Vitara New Model. Lakini ana Toyota Mark X ambalo limeelezwa anatumia mzazi mwenzake na jingine wanalotumia wazazi wake. Kama haitoshi, ana jumla ya nyumba nne jijini Dar es Salaam, tatu zikiwa Mbagala na moja Kigamboni huku akiwa na kiwanja kikubwa alichopewa na serikali baada ya kutangazwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wale wanaokipiga ndani ya Bara la Afrika.

Lakini hiyo unaweza kuona kuwa, Samatta anajua biashara, anaelewa soka lina mwisho hata kama bado ni kinda. Hivi karibuni, taarifa zinaeleza alinunua Bajaj 40 ambazo kama moja ni Sh milioni 6, basi maana yake ni Sh milioni 240 kwa zote na kuzikabidhi kwa familia yake kama sehemu ya biashara.

“Kweli kabisa, amenunua Bajaj 40, sema mzee (baba Samatta) hapendi kabisa kusema vitu hivyo kwa kuwa Samatta naye si mtu wa majigambo na anapenda mambo yake yaende kwa siri,” kilieleza chanzo ambacho ni memba wa familia ya mchana nyavu huyo ambaye msimu huu ameshaifungia timu yake mabao tisa.

Kuhusiana na hilo la Bajaj, baba Samatta ambaye ni mshikaji sana, alisema: “Familia ina mambo mengi sana, nafikiri mengine tuyaache yafikie kwetu.

Lakini Samatta anajua nini maana ya biashara na si vizuri kusema kila kitu.” Samatta alichipukia kisoka maeneo ya Mbagala kabla ya kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Daraja la Kwanza wakati Mbagala Market iliyo chini ya Mo Dewji ikipanda Ligi Kuu Bara naye akawa mchezaji bora.

Alijiunga na Simba ambako hakudumu sana kwa kuwa karibu robo msimu alibaki nje akidai kulipwa gari ambalo aliahidiwa kwenye mkataba. Baadaye Simba walitimiza, naye akaingia uwanjani na miezi michache baadaye, TP Mazembe wakafungua macho baada ya kumuona katika mechi mbili za Lubumbashi na Dar es Salaam.

Comments are closed.