The House of Favourite Newspapers

Balozi Wa Kenya: Adui wa Tanzania na Kenya Ni Corona Virus – Video

0

 

 

BAADA ya kutokea kwa sintofahamu ya kufungwa kwa mipaka kati ya Tanzania na Kenya, hatimaye ubalozi wa Kenya umefungukia suala hilo.

 

Wiki kadhaa zilizopita, kuliibuka malalamiko mengi hasa kutoka kwa madereva wa Tanzania waliowekewa kizingiti cha kuingia nchini Kenya huku wakidai wanabaguliwa na kuwekewa vizingiti visivyokuwa na mantiki kwa kisingizio cha kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 unaoenezwa na virusi vya Corona.

 

Madereva kwenye mipaka wa Holili Kilimanjaro, Horohoro Tanga na ule wa Namanga Arusha walilalamikia kubaguliwa na Wakenya kwa madai kuwa wana virusi hivyo na kuzuiwa kuingia nchini humo bila kuelezwa sababu za msingi.

 

Akizungumzia suala hilo leo Mei 19, 2020  jijini Dar, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu alisema ametumwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuwaambia Watanzania kwamba wao ni ndugu na kwamba hawana sababu ya kuwekeana vikwazo.

 

Alisema kilichotokea kwenye mipaka hiyo ni suala zima la mapambano dhidi ya virusi vya Corona na kwamba wao hawakuzuia magari ya mizigo yasiingie au kufanya biashara bali wamechukua hatua za kuzuia watu wengine wasiingie kupunguza maambukizi.

 

“Hatujafunga magari na safari za mizigo katika eneo la Afrika Mashariki, unaweza kwenda wakati wowote,” alisema Balozi Kazungu.

 

Balozi huyo alisema, tatizo la kuzuiwa kwenye mipaka liliwakuta hata wao kuingia nchini Uganda ambao walifunga mipaka yao na wakajadili pamoja namna bora ya kuweza kuendelea na biashara.

 

“Kuanzia wiki mbili zilizopita tulikaa na Waganda na tukasema hakuna dereva anatoka Mombasa au Nairobi kuelekea mipakani kama hajapimwa na kuonekana yupo negative na hicho ndicho tunachokizingatia,” alisema balozi huyo.

 

Tamko hilo la Kenya limekuja ikiwa ni siku moja tu mara baada ya wakuu wa mikoa ya Tanga, Martin Shigella na Anna Mghwira wa Kilimanjaro kutangaza kufunga mipaka iliyoko kwenye maeneo yao na kuzuia magari yote ya Kenya kuingia nchini.

 

“Hatuwezi kuruhusu madereva wa Kenya waingie watuletee Corona. Hivi karibuni tumewapima madereva wao karibu 19 tumewakuta wana Corona,” alisema Shigella na kuwaagiza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuruhusu magari ya nchi nyingine zote yaingie na kutoka nchini isipokuwa ya Wakenya.

 

Leave A Reply