The House of Favourite Newspapers

Bata La Ndani Ya Emirates, Hakuna England

0
Mhariri Kiongozi wa Gazeti la Championi, Saleh Ally akiwa amekaa katika benchi la Arsenal.

INAWEZEKANA uliishuhudia kwenye runinga mechi ya Ligi Kuu England kati ya Arsenal na Bournemouth kwenye Uwanja wa Emirates mjini hapa.

Kwa kuangalia mechi pekee ni vigumu kujua ubora au mambo mengine yaliyo kwenye uwanja huo unaomilikiwa na Arsenal.

Kawaida unapoangalia mechi, macho huishia mwisho uwanjani na viwanja vingi hufanana kwa mwonekano, katikati ya dimba.

Lakini unapoingia kwa undani zaidi utagundua mengi na hii ndiyo sababu ya Gazeti la Championi kufunga safari maelfu ya kilomita kwenda kuwatafutia wasomaji wake mambo ambayo hawakuwahi kuyajua hapo kabla.

Moja ya sehemu za kupumzika ndani ya Uwanja wa Emirates.

Uwanja wa Emirates ndiyo wenye mpangilio mzuri zaidi ukilinganisha na viwanja vingi vya mpira hasa vile vinavyomilikiwa na timu kubwa.

Emirates ambao ulianza kujengwa na kukamilika Julai 2006 una mfumo wa kisasa zaidi kama utalinganisha na viwanja kama Old Trafford wa Manchester United au Stamford Bridge wa mabingwa wa England, Chelsea.

Mgahawa ndani ya Emirates.

Championi limefika katika viwanja vyote hivyo na Emirates unaonekana kuwa na ubora kuzidi ulivyo wa Camp Nou wa Barcelona na hata Santiago Bernabeu wa Real Madrid za Hispania, hasa unapozungumzia mpangilio wa ndani.

Kwa upande wa mashabiki ambao unaingiza hadi watu 60,432 waliokaa vitini, utaona aina ya ukaaji ni bora zaidi, viti vina nafasi ya mtu na mtu kwa maana ya mbele na nyuma, yaani sehemu ya kuweka miguu kama utalinganisha na Stamford Bridge au Old Trafford.

Ukaaji wake, yaani aina ya yai, inampa mtazamaji nafasi ya kufaidi zaidi mpira kwa kuwa mfumo wake umekuwa wa kisasa zaidi kuliko mtazamaji kukaa kama ananing’ng’inia kama ambavyo umekuwa ukiona kwenye Dimba la Camp Nou. Ukiingia Emirates utaona tofauti kubwa zaidi.

Sehemu ya kupata vinywaji na chakula ndani ya Uwanja wa Emirates.

Lakini ndani ya uwanja huo, kuna hoteli maalum ambayo unaweza kuuita ni mgahawa lakini ukawa na ubora kuliko hoteli za nyota tano za Ulaya au hata nyumbani Tanzania.

Ukiingia kwenye mgahawa wa Diamond, hakika kweli ni almasi namna ulivyopangiliwa na umegawanyishwa katika maeneo mawili. Moja likiwa ni kwa ajili ya watu maarufu tu ambao wanahusika na klabu hiyo au wageni wao. Lakini sehemu ya pili ni ile ambayo hutumia wateja waliolipa VIP.

Kunakuwa na chakula maalum ambacho huwekwa kwa mfumo wa “bufee” na wakati wa mapumziko au kabla na baada ya mechi, watu hujiachia wanavyotaka wao.

Chumba cha watoa huduma wa Uwanja wa Emirates.

Ndani ya uwanja huo kama vilivyo viwanja vingi kuna ukumbi mkubwa ambao ni wa kisasa zaidi kuliko ule wa Old Trafford na ule wa Stamford Bridge na huu ni kwa ajili ya wachezaji mara baada ya mechi hukutana pamoja kwa ajili ya kinywaji kidogo na baada ya hapo hurejea majumbani kwao.

Sehemu maalum ya waandishi, ndani ya Uwanja wa Emirates kunakuwa na tofauti na kwingine pia. Kawaida karibu kila uwanja ndani yake una ukumbi wa kisasa kwa ajili ya waandishi wa habari kabla na baada ya mechi.

Pakuingilia hotelini ndani ya Uwanja wa Emirates.

Mwonekano wa Ukumbi wa Chelsea, unaonekana ni wa kizamani zaidi. Kunaweza kuwa na nafuu kwa ule wa Old Trafford ambao ulikarabatiwa upya miaka sita iliyopita.

Lakini ule wa Arsenal ni wa kisasa zaidi unaweza kuufananisha na ule wa FC Barcelona au Real Madrid ingawa huu unaonekana umetengenezwa hivi karibuni.

Kinachovutia zaidi kama ungekuwa mwandishi ni sehemu maalum ya waandishi kufanyia kazi kama ilivyo katika viwanja vingine lakini hii ya Arsenal ina uwezo wa kuchukua zaidi ya waandishi 200 wakafanya kazi zao na pia wamewekewa sehemu maalum ya kupumzikia baada ya mkutano.

Sehemu nyingine ya kupata vinywaji na chakula ndani ya Uwanja wa Emirates.

Chadema: Lissu Amevunjwa Mguu na Nyonga Lakini Jasiri, Tumuobee!

 
Kila wakati wa mechi kunakuwa na vinywaji na vitafunwa vimeandaliwa na wanaendelea na kazi yao huku kidogokidogo wanatupia “dawa”.
Ndani ya uwanja huo pia kuna sehemu zenye ukumbi mkubwa uliotengwa mara mbili na inawezekana kabisa kufanyika hata mikutano ya kimataifa.

Wakati wa ziara ya Championi kwenye uwanja huo, kulikuwa na mitihani ya kimataifa ikifanyika hapo na upande mwingine kulikuwa na usaili wa wafanyakazi takribani 200 waliokuwa wakipambana kupata kazi kupitia ukumbi huo mmoja wa kisasa.

Sehemu ya kuchukulia chakula.

Hivyo Arsenal pia imekuwa ikiingiza fedha kupitia kukodisha kumbi hizo mbili kubwa na za kisasa kabisa, ukiwa ndani unaweza usijue kama uko kwenye uwanja wa soka.

Mvuto wa uwanja huo, umefanya pia uwe unakodishwa kwenye matamasha mbalimbali ya muziki na hii ni kutokana na mazingira yake kuwa rafiki ndani na nje ya uwanja, hivyo kuwavutia wengi kukodi hasa ligi inapokuwa imesimama.

Gharama hadi uwanja huo unakamilika ni pauni milioni 390 (zaidi ya Sh trilioni 1) na kazi ya ujenzi ilifanywa na kampuni ya wataalamu wa ujenzi ya Populous kwa kushirikiana na mainjinia wa Kampuni ya Buro Happold.
Mazingira ya uwanja huo kwa nje ni rafiki sana kwa mashabiki kutokana nafasi yake ilivyo na ujenzi wake unavyorahisisha mambo kwa mashabiki kuingia na kutoka.

Raha zaidi, uko karibu kabisa na kituo cha treni cha chini cha Arsenal, hivyo kutoa nafasi kwa mashabiki wengi kuingia na kutoka haraka kufika au kuondoka katika eneo hilo la Holloway ulipo uwanja huo.

Kwa idadi ya watu, Emirates ni wa tatu baada ya Wembley unaomilikiwa na serikali na Old Trafford mali ya Manchester United. Lakini ni ubora, mvuto na muundo wa kisasa kwa England ukiacha Wembley, kwa viwanja vinavyomilikiwa na klabu, Emirates ndiyo uwanja wa kisasa zaidi kuliko vingine vyote katika Ligi Kuu England, mali ya klabu.

Na Saleh Ally, London | Championi Jumatatu

Leave A Reply