The House of Favourite Newspapers

BREAKING NEWS: Tundu Lissu Aachiwa kwa Dhamana (Video)

0
Tundu Lissu akiwasalimia wananchi waliofika mahakamani hapo.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, Tundu Lissu mapema leo asubuhi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ametoa uamuzi huo leo, Julai 27 akimtaka Lissu kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambapo kila mmoja atasaini bondi ya Sh10 milioni huku akipewa sharti la kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali maalum cha mahakama.

Aidha kesi yake imepangwa kusikilizwa Agosti 24 mwaka huu baada ya wadhamini wake kukamilisha taratibu zote za kumdhamini.

 

Lissu akipelekwa mahakamani.

 

 

Tundu  Lissu ambaye alikamatwa Alhamisi, Julai 20 mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati akijiandaa kuelekea Kigali, Rwanda kwenye kikao cha Chama cha Wanasheria cha Afrika Mashariki (EALS), alifikishwa Mahakamani hapo Jumatatu Julai 24 na kusomewa mashtaka  ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Serikali, kosa ambalo anadaiwa kulitenda Julai 17.

Julai 24, jopo la mawakili wanne wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa, Simon Wankyo, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo waliwasilisha hoja mahakamani hapo wakiomba Lissu anyimwe dhamana.

Jopo la mawakili 18 wanaomtetea Lissu, likiongozwa na Fatma Karume na Peter Kibatala liliomba mteja wao apewe dhamana.

Katika shauri linalomkabili, Lissu anadaiwa Julai 17 eneo la Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam alitoa maneno  ya uchochezi kuwa, ‘Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.’

 

NA DENIS MTIMA | GPL

====

VILIO, SIMANZI VYATAWALA KUAGWA KWA MTOTO NORAH

Lissu Aachiwa Huru, Kesi Yake Kuunguruma Agosti 24

Leave A Reply