The House of Favourite Newspapers

Celine Dion Apatwa Ugonjwa Usiotibika, Atuma Salamu kwa Mashabiki Wake

0
Mwanamuziki Celine Dion

WALE wahenga au tuwaite vijana wa zamani ukiwatajia jina la Celine Dion baadhi yao wanaweza kutokwa na machozi wakikumbuka walikuwa wapi na wanafanya nini wakati mwanamama huyo anawabembeleza kwa nyimbo na sauti yake tamu.

Baadhi ya nyimbo zake zinazoishi hata kama Celine Dion atatangulia mbele za haki ni pamoja na My Heart Will Go On, A New Day Has Come, That’s the Way It Is, The Power of Love, To Love You More na nyingine nyingi, muda umekwenda haraka mno!

Taarifa mbaya kwa vijana wa zamani ni kwamba yule kipenzi chao aliyekuwa akiwaburudisha wakati wa maakuli na kuwalaza unono; Celine Dion afya yake imeyumba.

Celine Dion amekumbwa na ugonjwa usiotibika

Celene Dion ambaye ni mzaliwa wa Canada mwenye umri wa miaka 54 anaweka wazi hali ya afya yake kwa kusema amegundulika kuwa ana ugonjwa usiotibika unaofahamika kama Stiff Person Syndrome (SPS), ambao ni ugonjwa wa neva.

Celine Dion ambaye amejizolea umaarufu mkubwa duniani kote amewaambia wafuasi wake milioni 5.2 wa mtandao wa Instagram kuwa, ugonjwa huo unaifanya misuli yake isimame bila kudhibitiwa na amekuwa akikabiliana na ugonjwa huo kwa muda mrefu.

Mara kadhaa ugonjwa huo umesababisha Celine Dion kushindwa kutembea na hata kuimba, hali itakayomlazimu pia kuahirisha kushiriki kwenye maonesho yaliyopangwa kufanyika Ulaya mwezi Februari mwaka 2023.

“Hivi majuzi nimegunduliwa kuwa na ugonjwa wa nadra sana wa neva unaoitwa Stiff Person Syndrome ambao kwa wastani huathiri mtu mmoja kati ya milioni moja.

“Kwa bahati mbaya, mikazo hii inaathiri kila nyanja ya maisha yangu ya kila siku, wakati mwingine husababisha ugumu ninapotembea na kutoniruhusu kutumia sauti zangu kuimba jinsi nilivyozoea.” amesema Celine kwa huzuni.

Leave A Reply