The House of Favourite Newspapers

Chenge: Sitaki Utani!

0
Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew John Chenge.

Mwezi mmoja na ushee ukiwa umekatika tangu aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya nne, William Ngeleja kurudisha fedha alizopewa na mmoja wa wamiliki wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, iliyotokana na zile zilizokwapuliwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew John Chenge ametoa mpya kuhusu ishu hiyo.

 

Chenge ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu, katika mgawo huo, alipewa kiasi cha shilingi bilioni 1.6, sawa na ilivyokuwa kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, ilisemekana naye alikuwa njiani kurejesha fedha hizo serikalini, kama alivyofanya Ngeleja.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka.

Risasi Mchanganyiko limemtafuta Chenge kwa siku kadhaa, likitaka kufahamu nini maoni yake juu ya rejesho lililofanywa na Ngeleja, lakini pia likitaka kufahamu kama naye ana wazo kama hilo.

 

Alipopatikana kupitia simu yake ya mkononi mwishoni mwa wiki iliyopita, alisikiliza kwa makini kuhusu alichoambiwa, lakini alipotakiwa kujibu, alisema; “Unajua ngoja nikuambie, katika maisha yangu huwa sitaki utani, eeeh kwa hiyo kwa suala hilo naomba nikushukuru sana na kwa heri,” alisema kwa kifupi Chenge.

 

Juhudi za Risasi Mchanganyiko kutaka kusikia zaidi kutoka kwa mbunge huyo wa Bariadi zilikwama baada ya simu kutopolewa.

 

Baada ya kupata majibu hayo kwa ufupi, ilikuwa ni zamu ya Mbunge wa Muleba Kusini, Mama Anna Tibaijuka, ambaye katika mgawo huo naye alipatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya IPTL ambaye kwa sasa yupo rumande akikabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi.

 

Akionekana mchangamfu, mbunge huyo alisema maneno mengi yenye kuumiza yamesemwa juu yake kuhusiana na suala hilo, hivyo anawaacha binadamu waendelee kuzungumza wapendavyo, lakini mwenye ukweli ni yeye.

 

“Maneno yamekuwa ni mengi sana kwa kweli, nimesemwa kwa kila baya unalolijua, lakini nilichagua kukaa kimya na kuwaacha watu waseme kwa ufundi wao, maana huwezi kuwazuia watu kusema au kuwachagulia waseme nini, kuhusu Escrow naogopa na actually sitaki kuzungumza kwa undani sana maana suala lenyewe liko mahakamani, tuache kama lilivyo,” alisema mbunge huyo ambaye pia amewahi kufanya kazi Shirika la Makazi Duniani la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT).

 

Chenge na Tibaijuka walikuwa ni miongoni mwa watumishi waandamizi wa serikali, waliopewa mgawo katika fedha hizo zilizoibua mzozo mkubwa wa kimasilahi, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini wakati huo, David Kafu
lila kutoa hoja bungeni, akisisitiza kuwa fedha hizo zilikuwa ni za umma, huku vigogo wengi, wakiwemo baadhi ya mawaziri, wakisema hazikuwa za umma.

 

Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa baada ya kuwepo kwa mgogoro wa kimkataba kati ya Kampuni ya IPTL na Tanesco, shirika la umma ambao walikuwa ni wanunuzi wa umeme uliokuwa ukifuliwa na kampuni hiyo. Fedha hizo zilikwapuliwa wakati shauri hilo likiwa linaendelea mahakamani. Ngeleja, aliyepewa mgawo wa shilingi milioni 40.4 ambazo ziliingia katika akaunti yake Desemba 4, 2014 na Jumatatu ya Julai 19, 2017 akatangaza kuzirudisha fedha hizo kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

BRIGHTON MASALU, RISASI MCHANGANYIKO

Global TV Kenya: Ali Hassan Joho Atema Cheche Mtongwe Mombasa

Leave A Reply