The House of Favourite Newspapers

Dkt. Mpango, Nape, Nyalandu ‘Wavuruga’ Muhambwe

0


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Philip Mpango awahakikishia watu wa Kibondo kupata uhakika wa maji safi na salama kwa kujenga tenki kubwa la maji lenye ujazo wa lita milioni moja na laki tano

 

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akimnadi mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Muhambwe Dkt. Florence Samizi ili awe mbunge wa jimbo hilo ambalo linatarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo wa marudio kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Atashasta Justus Nditiye.

Akizungumza katika Mkutano huo wa hadhara uliyofanyika katika uwanja wa Taifa Kibondo Mjini, Makamu wa Rais ameeleza mipango ya Serikali ya kuondoa tatizo la maji lililokuwepo wilayani hapo.

“Na niwaambie kuwa ndani ya wilaya yetu hayati Rais aliyetangulia mbinguni aliahidi kujenga bwawa kubwa , na bwawa hili tayari tumeshaanza maandalizi ya kuleta tenki kubwa kwanza hapa lenye ujazo wa lita milioni moja na laki tano, ili wananchi wa Muhambwe wapate maji,” alisema.

Akigusia suala la barabara Mheshimiwa Mpango amesema; “Ahadi ya Chama cha Mapinduzi ni kujenga barabara ya Rami ambayo inaunganisha Mkoa wetu na Mikoa ya jilani ambayo ni Kagera , Tabora na Katavi”, alisema.

Dkt. Mpango pia alizungumzia kuhusu miradi ya kijamii ambapo amezungumza kuwa eneo la Busunzu kutajengwa kituo cha afya pamoja na barabara ya kilomita moja ya kwenda kwenye kituo hicho na akaongezea pia litanunuliwa na gari la kubebea wagonjwa Ili lisaidie eneo hilo.

Wengine waliotua Kibondo kumuombea kura ni Naibu katibu Mkuu wa CCM, Christina Mndeme, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani ambaye hivi karibuni amerejea CCM, Lazaro Nyalandu.

Pia, alikuwepo Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, Mbunge wa Kasulu ambaye pia ni waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na wengine.

 

Uchaguzi huo wa marudio unatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 16/05/2021 ambapo CCM inakabiliwa na upinzani mkali kupitia kwa mgombea wake, Julius Massabo huku Chadema wakigoma kushiriki uchaguzi huo.

Leave A Reply