The House of Favourite Newspapers

Exclusive… Usichokijua Kuhusu Pauline Zongo na Hukumu za Wabongo

0

NAMFAHAMU Pauline Zongo tangu enzi za East Coast Team akiwa kama First Lady wa kundi hilo akiwa na wasanii wengine kama AY, Crazy GK, MwanaFA, Abbas, Snare na wengine waliowaka mwishoni mwa mwaka 1999 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

 

Kundi hilo lilisikika na nyimbo nyingi kama Ama Zangu Ama Zao, Sister Sister, Itikadi, Komaa Nao, Piga Manati na nyinginezo. Baadaye Pauline alitamba na wimbo wake wa Ndoa ya Mateso (ambacho ni kisa cha kweli).

 

Najua Pauline alijinga na Bendi ya TOT kisha Kundi la Ndege Watatu akiwa na wenzake, Khadija Kimobiteli na Joan Matomolwa na baada ya hapo hakusikika tena.

 

Namfahamu Pauline kwamba chanzo cha hali yake kuwa hivyo si madawa ya kulevya kama baadhi ya Wabongo wanavyomhukumu!

 

Mwezi mmoja uliopita, Pauline alifanya mahojiano maalum na Global TV ambapo mwandishi Richard Bukos alimuuliza juu ya hali yake kwa sasa na ndipo alipofunua kisa cha ajali mbaya mno ya gari aliyoipata.

 

Kwenye ajali hiyo, Pauline alikuwa na mwenzake ndani ya gari na yeye akiwa ni dereva, mwenzake alifariki dunia papohapo na yeye alijeruhiwa vibaya mno kiasi kwamba hakuna aliyedhani kama atapona.

 

Pauline amefanyiwa upasuaji na kuwekwa chuma kwenye miguu yake yote na pia amefanyiwa upasuaji wa kukatwa utumbo baada ya vipandepande vya vioo vya gari kubaki mwilini mwake na kusababisha kuharibika kwa utumbo.

 

Pauline alipoteza meno kwa kiasi kikubwa na kwa sasa Pauline yupo kwenye mazoezi madogomadogo na pia amerekodi albam yeke yenye nyimbo nane kati ya hizo ana wimbo mmoja unaitwa Kama Si Wewe Mungu Nisingekuwa Hai Leo.

 

Wakati anafanya mahojiano hao, Pauline alionekana afya yake imetetereka na maisha yake yamepoteza muelekeo kama alivyoeleza mwenyewe kwenye mahojiano na mwandishi Richard Bukos na intavyu hii ipo Global TV;

 

BUKOS: Pauline kulikoni? Mbona kimya?

PAULINE ZONGO: Baada ya kundi letu (East Coast Team -ECT) kusambaratika mwaka 2006, nilijiunga na TOT Band. Mwaka mmoja tulikwenda kupiga kampeni ya kwanza na Kikwete (Rais Mstaafu) mwaka 2010 na ile ya Hayati Magufuli ya mwaka 2015.

 

Baada ya hapo nikaja kupata ajali mbaya sana ya gari na nilikuwa naendesha mimi mwenyewe, niliyempakia kwenye gari alifariki dunia palepale, kilichoniokoa mimi ni belt (mkanda) na Mwenyezi Mungu.

 

Nikavunjika miguu na meno, navaa sasa hivi meno na kuvua. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu aliweza kuniweka japokuwa nimekaa muda mrefu bila kutembea, muda si mrefu nimekaa, nimekaa sitaki kukumbuka yale kwa sababu nikayazungumzia mpaka nalia (analengwalengwa na machozi).

 

Isitoshe nikiangalia ni single mother, nina watoto wawili so ni mtihani f’lani ambao umekaa. Nilipo hapa miezi mitatu haijaisha nimetoka kufanyiwa opereshen, lakini Mungu bado ananiweka ina maana ana makusudi yake.

 

BUKOS: Ilikuwa shida ni nini?

PAULINE ZONGO: Nimefanyiwa operesheni nilikuwa na uvimbe tumboni, kuna baadhi ya vioo vilikaa tumboni baada ya ajali, vilipasukapasuka na vikaanza kunikata utumbo ndani kwa ndani hivyo ilibidi vitolewe.

BUKOS: Lakini unaendeleaje kwa sasa?

 

PAULINE ZONGO: Bado siko sawa ingawaje nimejikongoja narekodi album yangu mpya kidogo kidogo lakini siwezi kuperform sasa hivi kwenda stejini abda kwa kuibia ibia ujaribu, unapokuwa stejini unatumia nguvu ya kuimba na kucheza.

 

BUKOS: Zimewahi kuibuka tetesi umepotea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya!

PAULINE ZONGO: Mungu angekuwa binadamu, angekuja akashuka hapa akaongea, unajua kwa mfano ukasingiziwa kitu ambacho hujakifanya, inaumiza sana. Situmii bangi wala madawa ya kulevya. Pombe huwa nagusa nisiwe muongo.

 

Inauma sana kwa sababu mtu anaongea kitu kama hicho. Twende tukapime si kuna maabara! Tukimaliza mtanlipa? Unanichafua. Hivyo vitu sivitumii, siwezi kumuogopa binadamu hata wakiongea si poa tu, Mungu nimemshirikisha.

 

BUKOS: Vipi kuhusu familia?

PAULINE ZONGO: Mtoto wangu wa kwanza nadhani baba yake mnamjua ambaye ananisumbua kwenye matumizi ya mtoto. Mtunis Mohammed Yusuph, aliniachia yule mtoto akiwa na miaka miwili, sasa hivi ana miaka 13 kuelekea 14, nipo naye mimi na sipati matumizi yoyote.

 

Mtoto wangu wa pili nilizaa na mtu mwingine ambaye alikuwa anamuendeleza tukapishana dini, yeye ni Muislam, mimi ni Mkristo, lakini yupo na baba yake, baba yake alimchukua, ana miaka nane sasa. Baba yake siwezi kumtaja, amemchukua mtoto wake anaishi naye. Kwa hiyo nipo na huyu wa Mtunis.

 

BUKOS: Kipato sasa hivi unapata wapi ukiwa katka hali kama hiyo?

PAULINE ZONGO: Mungu ndiye anajua.

 

Najua Pauline ni mtumiaji wa vinywaji vikali tangu akiwa kwenye TOT na ndiyo maana yupo sober house kwa Pili Masana, lakini kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya, nitabisha hadi kesho! Si wote wanaopelekwa au kwenda kwenye sober house ni wahathirika wa madawa ya kulevya, wapo wenye uraibu (addictions) wa aina mbalimbali kama pombe, ngono, mawazo na mengine kedekede ya kisaikolojia!

Kilichonishtua ni juu ya hizi habari za madawa ya kulevya! Mungu ampiganie Pauline Zongo.

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO

Leave A Reply