The House of Favourite Newspapers

Harmonize Adaiwa Mshahara

0

MAMBO si mambo kwa upande wa staa wa muziki wa Bongo Fleva ambaye pia ni Mkurugenzi wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ ambaye kijana wake wa saiti (shamba boy), anamtuhumu kumdai mshahara wake wa miezi saba.

 

Kwa mujibu wa chanzo chetu, shamba boy huyo ni mlinzi wa nyumba ya Harmonize au Harmo anayojenga maeneo ya Mivumoni-Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Chanzo hicho kimeliomba Gazeti la IJUMAA kumfikishia taarifa Harmo kwani mtu wake huyo anapata taabu kwani ni mtu mwenye familia yake ambaye Harmo hajamlipa kwa miezi hiyo saba.

 

Ili kupata ukweli wa tuhuma hizo, Gazeti la IJUMAA lilifika eneo hilo na kukutana na shamba boy huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina.

Hata hivyo, mlinzi huyo alilihakikishia IJUMAA kwamba, Harmo hana nyumba nyingine zaidi ya hiyo ambayo ujenzi wake kwa sasa umesimama.

 

“Jamani hawa watoto kwa kujikweza hawajambo, Harmonize nyumba yake ya Madale ndiyo hii hapa mnayoiyona.

“Ninavyojua hana nyumba nyingine zaidi ya hii, lakini nina uhakika angekuwa na nyingine ningejua kwa sababu nipo karibu sana na mama yake,” anasema jamaa huyo.

 

Alipoulizwa juu ya madai yake ya kutolipwa kwa miezi saba, jamaa huyo alifunguka na kukiri kwamba, ni kweli ana miezi saba bila kulipwa mshahara wake wa kulinda na kutunza eneo hilo kama makubaliano ya awali yalivyokuwa.

 

“Aliyewaambia hajakosea hata kidogo, ni kweli hapa nilipo nina muda wa miezi saba sijalipwa pesa yangu na bado ninalinda.

“Ikumbukwe pia na mimi nina familia na watoto wanatakiwa kwenda shuleni na kulia kodi ya pango.

 

“Harmonize hana habari na mimi kabisa. Ukimwaambia anakujibu kuwa sijakutafuta mimi ulitafutwa na mama, kama una shida mwambie mama yeye ndiye ataniambia mimi eti kwa sababu mama yake ndiye anasimamia ujenzi.

 

“Kuna kipindi nilipatwa na msiba wa mwanangu wa kumzaa kabisa, nilimpa taarifa Harmonize juu ya suala hilo, lakini huwezi kuamini, Harmonize alinitumia shilingi elfu thelathini tu,” alilalama shamba boy huyo akiomba taarifa zimfikie Harmo kwani anateseka na maisha magumu.

 

Ili kujua ukweli juu ya jambo hilo, Gazeti la IJUMAA lilimtafuta mama mzazi wa Harmonize ambaye inasemekana ndiye msimamizi wa nyumba hiyo ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili mwanawe ambapo alisema kuwa, hawezi kuzungumza kitu chochote juu yake na hata kwa mtoto wake.

 

“Siwezi kumzungumza kitu chochote kinachomuhusu mwanangu na hata mimi mwenyewe, mimi siyo mtu wa mambo hayo hata kidogo, ndiyo maana ninaweza kupanda daladala na wala mtu asijue kama mimi ni mama wa Harmonize,” alisema mama huyo kisha akakata simu.

Imendikwa na Khadija Bakari na Memorise Richard.

Leave A Reply