The House of Favourite Newspapers

Harmonize, Diamond Wagawana Marekani

0

MUZIKI wa Bongo Fleva unazidi kupasua anga ambapo katika msimu huu wa majira ya joto (summer), kuna wasanii wawili wanaiwakilisha Tanzania katika shoo za kimataifa, IJUMAA lina ripoti kamili.

 

Mwanamuziki wa Tanzania, Nasibu Abdul au Diamond Platnumz, jana (Oktoba 8,2021) ameanza ziara zake za nchini Marekani kwa ajili ya shoo ambapo atalazimika kugawana mashabiki na msanii mwenzake wa Bongo Fleva, Rajab Abdul au Harmonize.

 

DIAMOND MZIGONI KUANZIA LEO

Wakati Diamond au Mondi akianzia shoo zake katika Ukumbi wa Buckhead Theatre huko Atalanta, Marekani, tayari Harmonize au Harmo ameshafanya yake huko Columbus, Ohio, Houston na New York tangu Agosti 15, 2021 alipoanza ziara zake nchini humo.

 

Taarifa za uhakika ambazo Gazeti la IJUMAA linazo zinaeleza kuwa, baada ya shoo ya Atalanta, Mondi au Simba atapita kwenye miji mingine mbalimbali ambapo atakwenda Washington DC mnamo Oktoba 10, 2021 kabla ya kuelekea Seattle mnamo Oktoba 15, 2021.

Baada ya hapo, Mondi ambaye ni C.E.O wa Wasafi Classic Baby (WCB) atakwenda Minneopolis siku ifuatayo; yaani Oktoba 16, 2021.

 

Miji mingine ambayo Mondi atasababisha balaa na kukutana na mashabiki wake ni pamoja na; New York, Louisville, Arizona, Houston, Boston na Dallas kisha ataendelea na shoo za Ulaya hadi mwanzoni mwa mwaka 2022.

Usiku wa kuamkia jana, Alhamisi, Mondi aliondoka Bongo ambapo alisindikizwa kwenye uwanja wa ndege na wasanii wake, Zuchu, Mbosso na Lava Lava ambao kwa pamoja walimtakia kheri katika safari hiyo.

 

NENO LA MONDI KWA WASANII WENZAKE

Kwa mujibu wa Mondi, wasanii wengi wanahofia kufanya mambo mapya kwa kwenda kufanya shoo za kimataifa au kujaribu mitindo tofautitofauti ili kuufikisha muziki huo mbali.

 

Hata hivyo, Mondi amewataka mashabiki wake nchini Marekani kufuatilia ratiba zake nchini humo ili wapate ladha tofauti ya muziki kutoka kwenye Taifa la Waswahili (Swahili Nation).

 

KONDE BOY ANAENDELEA KUKIWASHA

Kwa upande wake, Harmo au N’jomba Nchomali ambaye ni C.E.O wa Konde Gang Music baada ya kupitia mijini ya Columbus, Ohio, Houston na New York sasa ataendelea kukiwasha huko Los Angeles, Las Vegas, Idaho, Minnesota, Syracuse kisha atarejea New York kwa mara nyingine.

 

Hata hivyo, baadhi ya shoo za Konde Boy Mjeshi zilishindwa kuendelea huko Canada na Bara la Ulaya kutokana na majanja ya maambukizi ya UVIKO-19, lakini shoo zake za kimataida zitaendelea hadi Januari, 2022.

 

ZIARA ZA WASANII WENGINE AFRIKA

Mbali na Harmo na Mondi kugawana mashabiki wanaotumia Lugha ya Kiswahili kwa maana ya watu wanaotoka Mataifa ya Afrika Mashariki waishio nchini Marekani, pia msanii wa Nigeria, Wizkid naye alitoa ratiba ya shoo zake zilizoanza rasmi Septemba 10, 2021 na zitafikia ukingoni Januari 22, 2022 nchini Marekani.

 

Baadhi ya maeneo ambayo Wizkid atakafanya shoo ni Boston, MA, Chicago, Minneapolis, Las Vegas, Houston na Dallas.

STORI; KHADIJA BAKARI, DAR

Leave A Reply