The House of Favourite Newspapers

Kaseja: Mzee Mengi Alimzawadia na Jide

KIPA mwenye heshima kubwa kwenye soka la Tanzania, Juma Kaseja amesema kifo cha Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi ni pengo kubwa.

 

Dk. Mengi ambaye alikuwa mwanachama wa Yanga, alifariki Dunia usiku wa kuamkia Alhamisi katika Falme za Kiarabu nchini Dubai ambapo mwili wake unawasili jijini kesho Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi yakayofanyika kwao Machame, Kilimanjaro.

 

Kaseja ambaye anaichezea KMC, alisema Mengi alikuwa mtu wa msaada katika michezo pamoja na roho yake ya ukarimu aliyokuwa akiionyesha kwa jamii.

 

“Tutamkumbuka Mzee Mengi kwa mambo mengi aliyoyafanya kwanza alikuwa msaada mkubwa kwa jamii yetu hasa ya michezo ambapo alikuwa mlezi wa Serengeti Boys.

 

“Pia Mzee Mengi alikuwa ni mkarimu sana nakumbuka huko nyuma kampuni ya Samsung iliandaa shindano ambapo washindi tulikuwa watatu mimi, Lady Jay Dee na Mzee Mengi ambapo mimi na Jay Dee tulizawadiwa friji huku yeye akiwa amezawadiwa TV kubwa ya Samsung.

 

“Mwenzangu alimuomba wabadilishane yeye ampe Jay Dee TV kwa kuwa hatukuwa na uwezo wa kuzinunua kwa kipindi hicho na kisha zile friji tufanyie tathimini kisha na mimi nipate TV.

 

“Mzee Mengi alikubali bila hiyana hivyo ni kiasi gani alikuwa mtu mwenye upendo kwa watu,” alisema Kaseja ambaye aliwahi kuichezea Yanga.

Comments are closed.