The House of Favourite Newspapers

Lulu: Kupendwa na Mume Kila Mtu Ana Bahati Yake

0

ELIZABETH Michael almaarufu Lulu; ni mmoja wa mastaa wakubwa waliodumu kwa muda mrefu kwenye Bongo Movies ambaye ameanza kuigiza tangu akiwa mtoto mdogo wa umri wa miaka mitano.

Hadi leo, Lulu bado anang’ara kupitia jina lake hilo ambapo amekuwa akionekana runingani kupitia tamthiliya yake ya M.I.M.I pamoja na kwamba, kwa sasa tayari ni mke wa mtu na ni mama wa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Genesis Francis almaarufu G.

Lulu ambaye siku hizi wanapenda kumuita Mama G amempata mtoto huyo kwa mumewe Francis Ciza au Majizzo ambaye walifunga pingu za maisha siku ile ya Februari 16, 2021.

Gazeti la IJUMAA limefanya mahojiano maalum (exclusive) ya ana kwa ana na Lulu akiwa kwenye duka lake jipya la nguo linaloitwa Lizzydrip lililopo Sinza jijini Dar ambaye anafunguka mambo mengi kubwa ni namna ambavyo maisha ya ndoa yalivyo na kuwa mama pia;

IJUMAA: Habari za siku nyingi Lulu?

LULU: Kwema kabisa! Karibu Lizzydrip maana hapa ndipo nyumbani sasa hivi.

IJUMAA: Hongera sana kwa kujiongeza na kufungua kitu cha kukuingizia fedha.

LULU: Asante Mungu ni mwema kwa sababu kila kitu ni hatua na kwa vile mimi napenda sana kuvaa hivyo imekuwa kheri kabisa na wateja wangu watadamshi kama mimi.

IJUMAA: Unaweza kukaa dukani maana mastaa wengi wakifungua maduka kukaa dukani na kuendesha biashara zao ni mtihani, wewe umewezaje?

LULU: Hapana, mimi kwa kweli nitajitahidi ingawa nina mtoto mdogo, lakini ukweli ni kwamba wateja wakija watapata ushauri kutoka kwangu mimi mwenyewe.

IJUMAA: Kama mama, una majukumu mengine ya mtoto na sanaa, unafanyaje?

LULU: Kwa kweli mimi nacheza kotekote kwa sababu lazima nifanye vyote. Kama mama, mke na msanii na kila kitu lazima kisimame sehemu yake.

IJUMAA: Wengi wakikuangalia ni kama mwanamke ambaye hufanyi kazi kwa namna muda wote wanakuona unapendeza ukiwa huku na kule, hii imekaaje?

LULU: Watu wanaangalia tu pale kwenye mtandao, lakini kuna maisha mengine zaidi ya hayo na siyo kila kitu tukiweke kwenye mtandao, lakini ukweli ni kwamba nafanya kila kitu anachofanya mwanamke aliyekamilika, napika, nafua na vitu vingi sana.

IJUMAA: Uko kwenye uhusiano muda kidogo wa kimapenzi na mtu ambaye amekuoa, umewezaje maana watu maarufu wengi wao kudumu kwenye ndoa ni shida, nini siri yako?

LULU: Unajua kupendwa na mume kila mtu ana bahati yake, inawezekana iliniangukia mimi na pia maelewano ya mtu na mtu hivyo basi kuna mwingine atatamani sana kuwa kama wewe, lakini ukweli ni kwamba ni kuelewana mtu na mtu hivyo tu.

IJUMAA: Watu wakikuona wanaona wazi kuwa ni mwanamke ambaye unadekezwa na kupendwa au kupewa kila kitu unachokitaka, hii imekaaje?

LULU: (kicheko) kwa hiyo wanafikiria hivyo eeeh… basi na mimi nashukuru sana, sasa mke si lazima anadekezwa na mume wake!

IJUMAA: Mtoto amebadilishaje maisha yako?

LULU: Kwa kiasi kikubwa sana maana kuitwa mama siyo mchezo hata kidogo, kila kitu kinabadilika, mawazo na fikra na kingine kuitwa mama ni raha sana.

IJUMAA: Kuna kipindi unaandika jumbe mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinakuwa na maneno mazito kama mtu ambaye umeishi miaka mingi na kujua vitu vingi sana…unapata wapi au nani anakuandikia?

LULU: Mtu mwenye busara siyo lazima awe mkubwa hata kidogo au awe na mvi, ni jinsi ya mtu kichwani kwake na fikra zake zilivyo basi.

IJUMAA: Una mpango wa kuongeza mtoto mwingine?

LULU: Siyo mwingine, wengine hivyo bado sana.

IJUMAA: Siku hizi ni mara chache kuonekana sehemu mbalimbali za starehe, ni ndoa inakubana?

LULU: Kila kitu kinabadilika maishani kuendana na wakati hivyo hata kwangu pia.

IJUMAA: Asante Lulu kwa ushirikiano wako.

LULU: Asante sana na karibu tena na tena.

STORI NA IMELDA MTEMA

Leave A Reply