The House of Favourite Newspapers

Madini Mondi Yagharimu Nyumba 3 Za Kifahari

0

DIAMOND Platnumz; mwamba anayemiliki vitu vya bei mbaya ikiwemo mijengo ya thamani Tanzania na Afrika Kusini, hoteli ya kifahari, lebo kubwa ya muziki ya WCB na ndinga za bei mbaya kama BMW X6, Toyota Land Cruiser tatu, Rolls Royce moja na Cadillac Escalade mbili, lakini sasa amehamia kwenye kujichafua na madini mwilini, IJUMAA lina ripoti kamili.

Diamond au Mondi ambaye ni msanii mkubwa wa muziki barani Afrika, ameendelea kutisha kwa kuonesha jeuri ya pesa, akijichafua kwa madini ya vito vya thamani kama saa, pete, mikufu, meno na cheni za mamilioni kwenye mwili wake.

THAMANI

Maswali yamekuwa ni mengi, juu ya thamani ya vito hivyo ambavyo Mondi au Simba wa Tandale ameonekana akivivaa siku za hivi karibuni.

Baadhi ya wadau waliozungumza na Gazeti la IJUMAA juu ya kuchafuka madini kwenye mwili wake akiwemo Baba Levo wanasema kuwa, pesa alizotumia kwake ni za madafu tu, lakini ni za mamilioni ya shilingi za Kitanzania.

Hata hivyo, uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umejitahidi kuwafikia wahusika wanaojua hasa thamani ya madini anayojitundika Mondi ambapo kwa harakaharaka, kwa mtu mwingine anaweza kutumia kiasi hicho cha pesa kujenga majumba matatu au zaidi ya kifahari, lakini mwamba anatupia tu mwilini.

Kwa jumla, Mondi au Chibu hakuingia duka moja kununua vito hivyo ambavyo vinazua gumzo mjini.

Watu wa karibu wanaeleza kwamba, kuna kampuni kubwa tatu zinazohusika na uuzaji wa vito hivyo ambayo Simba wa Tandale ameyafikia na kutoa pesa kuvinunua ambazo ni Shohreh Customade, Ice Jewelz na Pristine Jewellers.

PETE

Mondi anavaa pete zinazojulikana kama Orbit Ring Rose Gold na Orbit Ring Rose White Gold; ambazo ni pete zilizotengenezwa kwa madini ya dhahabu zikiwa na uzito wa gram 18.8.

Kwa mujibu wa wataalam wa kampuni hizo kupitia kurasa zao za kijamii, pete hizo zinatengenezwa kwa madini yanayofanana, lakini utofauti wake unakuja kwenye rangi; pete moja ina rangi ya njano huku nyingine zikiwa nyeupe.

Inaelezwa kwamba, thamani ya pete moja ni Dola za Kimarekani 6,825 (zaidi ya shilingi milioni 16 za Kitanzania).

Aina nyingine ya pete anayoonekana nayo Mondi inajulikana kwa jina la Locked Star Ring White Gold ambayo imenakshiwa na umbo la nyota huku madini yaliyotumika kuitengeneza ni dhahabu.

Pete hiyo ina uzito wa gram 20.5 huku thamani yake ikitajwa kuwa ni Dola za Kiamrekani 7,515 (zaidi ya shilingi milioni 17 za Kitanzania).

SAA

Wakati akitumia zaidi ya shilingi milioni 33 kununua pete mbili, Chibu ametumia pesa ndefu zaidi kununua saa moja ya mkononi yenye madini ya chuma ambayo toleo la kwanza lilitoka mwaka 2015.

Taarifa za kitaalam zinasema kuwa, saa hiyo aina ya Rolex Datejust Watch ina thamani ya Dola za Kimarekani 27,326 (zaidi ya shilingi milioni 63 za Kitanzania).

Kama angeamua kununua viwanja maeneo ya Buza jijini Dar, angenunua mtaa mzima.

MENO

Mondi au Chibu Dangote anaingia kwenye listi ya mastaa wachache wanaomiliki meno ya thamani aina ya Gold Plated Girls yenye thamani kubwa duniani.

Anakuwa kwenye levo moja na mastaa kama Gucci Mane, Lil Wayne na Kanye West ambao wanayo au walishaonekana na aina hii ya meno.

Wataalam wa kampuni hizo wanabainisha kwenye kurasa zao za kijamii kwamba, meno hayo bandia yametengenezwa kwa madini ya dhahabu na almasi huku kila jino moja likiwa na thamani ya Dola za Kimarekani 181 (zaidi ya shilingi laki 4 za Kitanzania kwa jino moja na kwa seti mzima ni takriban shilingi milioni 11 za Kitanzania.

CHENI ZA MKONONI

Katika siku za hivi karibuni, Mondi ameonekana akiwa amevalia cheni tatu ndogo za mkononi ambazo kitaalam zinaitwa Shared Prong Setting Diamond Evening Bracelet ambazo zinafanana umbo na madini yaliyotumika kutengeneza cheni hizo ambazo ni almasi.

Wataalam wanataja thamani ya kila cheni moja kuwa ni Dola za Kimarekani 4,169 (zaidi ya shilingi milioni 9 za Kitanzania) kwa kila cheni moja ambapo kwa zote tatu ni takriban milioni 29.

Pia Mondi anamiliki cheni nyingine za mkononi zinazoitwa White Gold Plated Mens Iced Brecelate ambazo zimetengenezwa madini ya dhahabu nyeupe.

Thamani yake inatajwa kuwa ni Dola za Kimarekani 1,430 (zaidi ya shilingi milioni 3 za Kitanzania).

CHENI ZA SHINGONI

Kwa wanaomfuatilia Mondi watakuwa wamemuona akiwa amevalia cheni kadhaa, lakini moja ni kubwa yenye alama ya kichwa cha simba na maandishi yanayosomeka; ‘SIMBA’ ambayo wengine wanaihusisha na mambo ya Freemasons.

Kwa mujibu wa wataalam, cheni hiyo inaitwa Lion Head Gold and Diamond Chain ambayo imetengenezwa kwa madini mchanganyiko wa almasi na dhahabu na inatajwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani 48,000 (zaidi ya shilingi milioni 111 za Kitanzania).

MONDI: ACHENI KUVAA BANDIA

Mwenyewe Mondi anasema; “Acheni kuvaa mikufu bandia wavulana wadogo, kuna saratani.”

JUMLA

Kwa jumla ukiachana na cheni mbili za shingoni ambazo thamani imekuwa ngumu kupata, Mondi anavaa vito vya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 za Kitanzania ambazo ukisema ununue pikipiki utakuwa na zaidi ya bodaboda 100 huku ukisema ununue nyumba za milioni sabinisabini, basi utapata tatu za kifahari nje kidogo ya Jiji la Dar esSalaam.

STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR

Leave A Reply